PAMOJA na Serikali kuweka malengo mazuri ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, wabunge wamesisitiza kuwekwa utaratibu usio na urasimu kwa wawekezaji. Hii ni kutokana na utaratibu wa sasa kuwa na vikwazo vingi vinavyokimbiza wawekezaji.
Aidha, wabunge hao wameishauri serikali kutumia vyema rasilimali na malighafi zilizopo katika kuijenga sekta hiyo ya viwanda ili mafanikio ya viwanda hivyo yasiishie tu kwenye kuongeza ajira bali kuinua uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Pamoja na hayo, wabunge hao, wameisisitizia Serikali juu ya umuhimu wa kuanzisha kituo kimoja (one Stop center) kwa ajili ya kutoa huduma zote katika sehemu moja kwa wawekezaji jambo litakaloongeza vivutio kwa uwekezaji lakini pia kuwarahisishia wawekezaji hao kufanikisha kiurahisi taratibu za kuwekeza nchini.
Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliyowasilishwa juzi na waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema ni wakati sasa kwa serikali kuondoa vikwazo vyote vya uwekezaji ili kutimia ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Alitoa mfano wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania iliyotolewa Aprili, mwaka huu inayobainisha kuwa uzalishaji viwandani umeshuka kutoka dola za Marekani milioni 1.4 mpaka dola za Marekani 870,000, usafirishaji bidhaa nje umeshuka kwa dola za Marekani milioni 80, bidhaa za samaki dola za Marekani milioni 20 na usafiri na mawasiliano -21.6.
Aidha, alisema usafirshaji wa bidhaa za mazao ya asili nao ulishuka bidhaa pekee iliyokuwa ni korosho kutokana na kuongezeka kwa bei, tumbaku imeshuka kutoka Dola za Marekani milioni 343 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 281 mwaka huu, pamba imeshuka kwa Dola za Marekani milioni 10, kahawa Dola za Marekani milioni tisa na karafuu kwa Dola za Marekani milioni 13.
Tatizo ni sera za kodi kutotabilika, “sheria ya uwekezaji kifungu namba 19 tumeibadilisha mwaka 2009 kwa kuifuta, tukaibadilisha mwaka 2010, 2012, 2014 na 2015 tunafuta na kuruidisha wakati ni nchi moja, tunakimbiza wawekezaji kwa kuwa hatutabiriki,” alifafanua.
Alisema pia kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia mazingira ya uwekezaji nchini ni magumu, kwani ili uwe na kiwanda cha maziwa lazima uwe na nyaraka zaidi ya 10. Alitaja maeneo ambayo nyaraka hizo inabidi mwekezaji azitafute na kuwa nazo jambo linaloongeza urasimu na ukiritimba katika uwekezaji nchini kuwa ni Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA), Wakala wa Usajili Biashara na Utoaji Leseni (BRELA), Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Akizungumzia suala la kodi, Bashe alisema serikali inabidi kufikiria kupunguza utitiri huo wa kodi ikiwa ni pamoja na kuzindoa zile zisizo za lazima. “Kwa mfano kuzalisha square feet ya ngozi Tanzania ni senti dola za Marekani senti 14 wakati Ethiopia ni dola za Marekani senti nane na India dola za Marekani senti saba. Tutawezaje kushindana?”
Kwa upande wake, mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto, alisema itakuwa ndoto kwa Tanzania kwenda kwenye uchumi wa viwanda bila kufungamanisha sekta nyingine zikiwemo za kilimo na uzalishaji wa malighafi.
Alisema kwa hali ilivyo inaonyesha wazi kuwa viwanda vingi nchini vimepunguza uzalishaji kutokana na ukweli kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana Tanzania iliuza bidha za viwanda zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.4 ambapo pia takwimu za mwaka huu zinaonyesha mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameshuka kwa dola za Marekani milioni 500.
Naye mbunge wa Hanang, Mary Nagu (CCM) alisema bado Serikali ya awamu ya tano imepiga hatua nzuri mpaka sasa katika kutekeleza sera ya maendeleo ya mwaka 1996 ambayo imefanikisha viwanda kukua nchini kwa asilimia 7.8.
Nagu ambaye aliwahi kuwa Waziri pia wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, aliitaka Serikali kuendelea kutekeleza Mradi wa Muunganisho wa Ujasiriamli Vijijini (MUVI) uliopo chini ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na kuanzisha miradi mingine kama hiyo kwani imeonyesha mafanikio katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
Pia mbunge huyo, aliishauri serikali kuwa na eneo moja la kutekeleza taratibu zote za kiuwekezaji ili Mawaziri EAC wataka mfumo mmoja wa elimu Wabunge: Wawekezaji wapunguziwe vikwazo kuondoa urasimu uliopo kwa wawekezaji ambao hulazimika kutumia muda mwingi kutekeleza masharti ya uwekezaji tofauti na nchi nyingine za jirani.
Mbunge wa viti maalum, Gimbi Masaba (Chadema), aliishauri serikali ianze kuchukua hatua dhidi ya viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo mpaka sasa havifanyi kazi na vingine kugeuzwa maghala kwa kuhakikisha vinanyang’anywa kutoka mikononi mwa wawekezaji na kupewa wawekezaji wapya watakaovifufua.
Wengi wabunge wa wabunge waliochangia pamoja na kuipongeza serikali kwa hatua ya kuijenga Tanzania ya viwanda, pia wameitaka serikali ipeleke viwanda katika majimbo yao kutokana na majimbo hayo kujaaliwa kuwa na malighafi nyingi zinazotosheleza katika uwekezaji wa viwanda.
0 comments:
Post a Comment