Serikali imelionya baraza la madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji
kuacha mara moja kushiriki kwenye Mpango wa Kimataifa wa uendeshaji wa
shughuli za serikali kwa uwazi (OGP), ambao serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imejitoa.
Onyo
hilo limetolewa leo bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na
Utawala Bora, Mh. Goerge Mkuchika wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe lilitoka kujua kauli ya serikali
kutokana na ushiriki wa Manispaa hiyo kwenye mpango huo.
“Serikali inazo taarifa kuwa Manispaa ya Kigoma Ujiji mpaka sasa
inawasiliana na OGP na OGP wamemwandikia barua Waziri wa mambo ya Nje
kwamba wana nia ya kuendelea kushirkiana na nyie, sasa nataka niionye
Manispaa ya Kigoma Ujiji waache mara moja kuwasiliana na OGP”.
Aidha Waziri ameitaka Manispaa hiyo kutekeleza maamuzi ya serikali na
endapo itaendelea basi serikali itachukua hatua kali ambazo ni kuvunja
baraza la madiwani na kuweka Tume ya Manispaa.
Waziri pia ameeleza kuwa taratibu za OGP zipo wazi kuwa nchi ikijitoa
moja kwa moja ushiriki wa wanachama wengine kutoka ndani ya nchi husika
unakuwa umefika kikomo hivyo Manispaa hiyo inavunja kanuni za nchi.
Tanzania imejitoa kwenye Mpango wa Kimataifa wa uendeshaji wa
shughuli za serikali kwa uwazi (OGP), ambao imedumu kama mwanacham kwa
miaka minne tangu ilipojiunga Septemba 21 mwaka 2011.
0 comments:
Post a Comment