Wananchi wa Kisiwa cha
Soswa halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wamewatupia mpira
walimu waliojikuta wamelala nje kwa madai ya imani za kishirikina kuwa
ni tukio la kutengenezwa.
Wakizungumza kwenye mkutano
wa hadhara ulioitishwa jana Alhamisi kwa dharura kujadili suala hilo
lililojitokeza usiku wa kuamkia Novemba 15, mwaka huu, katika viwanja
vya shule ya msingi Soswa wananchi hao walisema tukio hilo ni la
kutengenzwa ili kuishinikiza Serikali iwape uhamisho kutokana na
mazingira magumu wanayokaa.
Mzee wa kisiwa hicho,
Mashinga Boniphace (80) alisema hakuna ukweli juu ya tukio hilo kwani
yeye pamoja na wazee wenzake waliangalia vibuyu na damu iliyokuwa
imetapakaa ndani ya nyumba za walimu hao sio ya kishirikina.
“Walimu
hao waliamua kuua ndege aina ya nyagenyange ili na kutapakaza damu hizo
ndani ya nyumba zao pamoja na kwenye vibuyu ili kushinikiza uongozi wa
juu kuwahamisha kutokana na juhudi zao za kuhama kugonga mwamba,”alisema
Boniphance
Kauli ya mzee huyo wa mila ilipingwa na
mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mjula Magafu ambaye alisema suala hilo
liangaliwe kwa kina kwakuwa limezua sintofahamu ndani ya kisiwa hicho na
Taifa kwa ujumla.
Alisema kama walimu ndio walitengeneza tukio hilo wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kudanganya umma.
“Hapo
awali lilipotokea tukio la nyumba zao kupondwa mawe walimu wote
waliondoka na kubaki wawili ambapo hakukuwa na kitendo kama hicho,
baadaye walimu waliokuwa wamesusia akiwemo mwalimu Daudi Shule na Wape
Kisimu kitendo hicho kilijirudia tena na sasa wameamua kutengeneza tukio
la kulazwa nje, tunapaswa kuchunguza kwa kina,” alisema Magafu
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwananchi walisema tukio hilo limewaathiri kimasomo hivyo kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Mwanafunzi
wa darasa la tano, Malisela James aliiomba jamii ikubali kuwa walimu
hao wamefanyiwa vitendo vya kishirikina na kwamba watafute namna ya
kukukomesha ili kuwapa fursa ya kuendelea kusoma.
Mwenyekiti
wa kamati ya shule, Lidia Buluba alilaani kitendo hicho ambacho
kinahisishwa na imani za kishirikina huku akiwatupia lawama baadhi ya
walimu waliotengeneza jambo hilo ili wapatiwe uhamisho kwa madai kuwa
mazingira wanayoishi si mazuri.
Mwalimu Daudi Shule
ambaye anapatiwa matibabu ya asili katika kijiji cha mwangakia yeye
alidai alinyolewa sehemu za siri, mwalimu Ernest Katunzi alithibisha
kwa kumwona sehemu hizo kuwa amenyolewa pamoja na mwalimu Wape Kisumo
aliyonyolewa nywele kichwani kwa pamoja walisema kuwa wanafanyiwa
vitendo vya kishirikina hata kipindi wanapondwa mawe jamii hiyo
haikuamini.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Petro Lukas
alisema maneno yanayosemwa na jamii hawawezi kuyaamini na haamini kama
walimu wametengeneza mazingira ya tukio hilo ili wahame kwa kuwa kazi
yao ni kufundisha.
Mtendaji wa Kata ya Bulyaheke, Musa
Mwilomba alisema kuwa anaiomba jamii kutokutupiana mpira juu ya tukio
hilo na kwamba wanatakiwa kusameheana na kusahau kilichotokea ili kuanza
sura mpya na walimu waendelee kufundisha.
Mkaguzi wa
shule wilayani Sengerema, Elly Msulu aliyefika katika Kisiwa cha Soswa
kupata ukweli juu ya tukio hilo aliitaka uchunguzi zaidi ufanyike kujua
ukweli wa tukio hilo na watakaobainika hatua kali za kisheria dhidi yao
zitachukuliwa huku akiwaomba walimu kuwa wavumilivu wakati suala hilo
linatafutiwa ufumbuzi.
0 comments:
Post a Comment