Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Tuesday, December 26, 2017

WB:Uchumi Rwanda kukua kwa 17% kila mwaka.

RIPOTI ya Benki ya Dunia kuhusu uchumi wa Rwanda, inakadiria kuwa hadi mwishoni mwa mwaka huu, ukuaji utaongezeka hadi asilimia 5.2. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, uchumi wa nchi hiyo ulikua kwa asilimia 3.4.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Rwanda, Edouard Ngirente amesema kuwa katika miaka saba ijayo, uchumi wa nchi hiyo unakadiriwa kukua kwa asilimia 17 kila mwaka. Inakisiwa kuwa kasi ya ukuaji itaongezeka mwakani na mwaka 2019 kwa kuwa, uwekezaji katikasekta ya umma na ya binafsi unaongezeka na tija kwenye kilimo inaongezeka.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), uchumi wa Nauru, Ethiopia, Turkmenistan, Qatar, China na Uzbekistan ndiyo uliokua kwa kasi zaidi mwaka huu. Pia uchumi wa Rwanda unakua kwa kasi, na kwa miaka kadhaa sasa umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia nane kwa mwaka. Mwaka jana uchumi huo ulikua kwa asilimia 5.9 na inakisiwa kuwa mwaka huu utakua kwa asilimia 6.2.
Kasi ya ukuaji uchumi Rwanda inachangiwa na mambo kadhaa ukiwemo uimara wa sera na taasisi. Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu ushindani, uchumi wa Rwanda ndiyo wenye ushindani zaidi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na ni miongoni mwa nchi tatu za juu kwa ushindani wa uchumi Afrika Kusini ya Jangwa la Sahara.
Ngirente pia alisema katika miaka saba ijayo, Serikali itaongeza kasi ya maendeleo ya majiji madogo ili kuhakikisha asilimia 35 ya Wanyarwanda wanaishi huko ifikapo mwaka 2024. Kwa sasa asilimia 17.5 ya wananchi hao, wanaishi kwenye maeneo hayo.
Ngirente alisema hayo kwenye Baraza la Majadiliano la Taifa, wakati akiwasilisha Mkakati wa Taifa kutoka kwenye mabadiliko. Wajumbe 2000 walihudhuria baraza hilo akiwemo Rais Paul Kagame. Mkakati huo unaanza kutekelezwa mwaka huu hadi mwaka 2024.
Ngirente alisema, majadiliano hayo ni muhimu ili kutathmini nchi imetoka wapi na isonge mbele vipi na kila mtu atambue nafasi yake kwenye safari hiyo. “Ajenda ya Serikali inalenga maendeleo endelevu na mabadiliko ya watu wetu kwenye maeneo makubwa matatu; uchumi, jamii na uongozi. Rwanda imedhamiria kuendeleza sekta binafsi na kuwa na uchumi wenye ufahamu,” alisema.
Ngirente alisema, pamoja motisha kuvutia watu kwenye majiji, Serikali itaongeza viwanda na huduma nyingine nchini kote, hivyo kuongeza uwezo wa nchi kuuza nje. Serikali ya Rwanda pia ilisema katika miaka saba ijayo, vijana watapewa kipaumbele na itaongeza kiwango cha ujuzi kwenye sekta zote ili kundi hilo liandaliwe zaidi kwa soko la ajira. Kwa mujibu wa Ngirente, mkakati wa taifa pia unazingatia ukuaji wa kilimo na kwamba, jambo hilo litajumuishwa na mikakati ya kulinda mazingira.

0 comments:

Post a Comment