Maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usalama Barabarani (NTSA) pamoja na
Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya wametoa ushauri ambao unaweza kukufaa
sana wakati huu wa mvua.
- Fahamu kwamba wakati wa kiangazi,
vumbi, mchanga na taka za aina mbalimbali hurundikana barabarani. Mvua
inaponyesha, husababisha barabara kuwa telezi na kwa hivyo ukiwa na gari
ni muhimu kutoendesha gari lako kwa mwendo wa kasi kupindukia kwani
gari likiteleza utashindwa kulidhibiti gari lako kwa urahisi.
- Kwa sababu ya maji, huwa vigumu sana
kupiga breki wakati wa mvua na hivyo hatari ya mwenye gari kumgonga
anayetembea barabarani huwa juu. Unashauriwa kutoendesha gari kwa mwendo
wa kasi.
- Kwa sababu ya mvua, wapita njia mara
nyingi hutembea wakiwa wameinamisha vichwa chini na huenda wasilione
gari linapokaribia. Wenye magari wanashauriwa kuwa makini zaidi
wanapofika kwenye vivuko barabarani au wanapomuona mtu akivuka barabara.
Kwa wanaotembea kwa miguu, wanashauriwa kutumia vivuko vilivyotengwa na
kuchukua tahadhari zaidi pia.
- Kwa wenye magari, iwapo barabara
imefurika maji, ni vyema kutafuta barabara nyingine ya kupitia badala ya
kujaribu kupitia ndani ya maji. Huwa vigumu kukadiria kina cha maji
barabara inapofurika.
- Wakati mvua inaponyesha, wenye magari
wanatakiwa kuwasha taa kuwawezesha kuona mbele na pia kutokaribia sana
magari yaliyo mbele yao. Maji yanayorushwa na gari lililo mbele yanaweza
kutatiza mwenye gari iwapo atakuwa karibu sana. Ushauriwa kufuata
kanuni ya sekunde 3, hicho ndicho kipindi kinachochukuliwa na binadamu
kuona jambo na kuchukua hatua. Usipofanya hivi, kufikia wakati unapoona
aliye mbele yako amesimama na kuchukua hatua utakuwa tayari umesababisha
ajali.
- Breki za gari huathiriwa na maji, kwa
hivyo unapoendesha gari eneo lenye maji, ni vyema kuendesha gari kwa
mwendo wa polepole. Hii itaziwezesha breki kukauka.
- Madereva wanashauriwa pia kutumia mikono yao miwili kudhibiti mwelekeo wa gari kuhakikisha wanadhibiti vyema gari.
- Wapita njia, waendesha baiskeli na
waendeshaji pikipiki wanashauriwa kuvalia mavazi yanayoweza kuonekana
vyema au mavazi yanayoweza kuakisi mwanga. Haya yatamuwezesha mtu
kuonekana na madereva na kumpungushia mtu hatari ya kugongwa.
- Usiendeshe gari lako ndani ya maji
yanayosonga, yawe kwenye mifereji au kwenye mto. Huwa vigumu sana
kukadiria nguvu ya maji. Magari mengi husombwa na maji madereva
wakijaribu kuvuka mito au wakitumia madaraja yaliyofurika maji. Mvua pia
hudhoofisha madaraja, jambo ambalo huenda usifahamu. Daraja linaweza
kubomolewa bila ufahamu wake wewe nawe ukaingia mtoni ukitarajia daraja
bado lipo. Maji ya kina ya futi moja yanaweza kusomba gari lako. Kwa
binadamu anayetembea, inchi sita za maji zinaweza kukusomba.
- Ukiwa na gari lako, hakikisha
vipangusia kioo vya gari lako vinafanya kazi. Hili litakuwezesha
kupangusa kioo na kuona mbele unapokuwa barabarani.
- Iwapo una gari na limeanza kuteleza,
achilia mafuta na kulielekeza gari upande ambao unateleza. Ukianfanikiwa
kudhibiti gari, anza kulainisha magurudumu tena na kurejea barabarani.
Hakikisha kwamba unabaki kuwa tulivu na usichukue hatua yoyote ghafla.
- Usiende kwa mwendo wa kasi. Iwapo una
safari ya mbali, anza mapema kuhakikisha kwamba haukumbwi na shinikizo
la kutaka kwenda kwa kasi ndipo ufike.
- Unapokuwa unaendesha gari,
usishawishike kutumia simu yako au kufanya jambo lolote ambalo
litakuzuia kuwa makini ukiliendesha gari.
- Iwapo utakuwa safarini, usiegeshe gari lako au kuanza kufanya shughuli zako karibu na mto wakati wa mvua.
- Ni vyema kusikiliza vituo vya redio na
runinga kujifahamisha kuhusu yanayojiri na ni wapi mvua kubwaimenyesha
au mafuriko kutokea.
- Usitembee kwenye maji au maeneo yenye
matope ambayo kuna uwezekano kwamba kuna nyaya za umeme ambazo
zimeanguka. Nyumba yako ikifurika maji pia, hakikisha umezima stima.
- Iwapo unatembea kwa miguu, tumia fimbo au kijiti kukadiria kina cha maji.
- Mafuriko yakitokea eneo ulipo, mara moja kimbilia maeneo yaliyo juu na salama. @BBC
0 comments:
Post a Comment