Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Sunday, June 11, 2017

Diwani wa Iganjo aapishwa baada ya kushinda Rufaa ya kesi iliyomkabili tangu 2015.

Siku mbili baada ya kuapishwa, Diwani wa Iganjo katika Jiji la Mbeya (Chadema), David Mwangonela anatarajia kulipwa kitita cha zaidi ya Sh6 milioni zikiwa ni posho za kila mwezi za udiwani ambazo hajapokea kwa kipindi chote kabla ya kuapishwa.

Mwangonela anatarajia kulipwa fedha hizo ikiwa ni haki yake kwa miezi hiyo, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kabla ya kushinda rufaa Desemba, 2016 na kurejea uraiani.

Mwanasheria wa Jiji la Mbeya, Davis Mbembela alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hii kuhusu stahiki anazostahili kupewa diwani huyo baada ya juzi kuapishwa.

Diwani huyo alifungwa jela siku chache baada ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mbembela alisema Mwangonela ana haki ya kulipwa posho ya kila mwezi kuanzia alipochaguliwa mwaka 2015 isipokuwa posho za vikao na kamati kwa vile hakuwapo kwenye orodha.

“Posho za kwenye vikao na kamati hizo hatapata kwa vile hakuwa mshiriki, lakini ile ya kila mwezi ni haki yake atapewa kama kawaida kwa mujibu wa sheria,” alisema mwanasheria huyo.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, Mwangonela alishinda lakini Novemba 17, 2015 alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya kwa kosa la kuvunja ghala na kuiba magunia ya ngano mali ya Chuo cha Utafiti na Kilimo Uyole, hivyo kushindwa kuapishwa.

Hata hivyo, Mwangonela alikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo Mahakama Kuu ambako alishinda baada ya mahakama kumuona hana hatia bali alikuwa amepakaziwa.

Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ilitengua kifungo hicho Desemba 16, 2016, huku diwani huyo akiwa ametumikia kifungo kwa takriban mwaka na mwezi mmoja.

Awali, Mwangonela alipaswa kuapishwa Machi 9, lakini uliibuka mvutano, hivyo kikao kilivunjika kutokana kutofikia mwafaka kwa pande za madiwani wa Chadema na uongozi wa Jiji la Mbeya kupitia mwanasheria wake, Mbembela.

Katika kikao hicho, madiwani hao walitaka mwenzao aapishwe kwa kuwa kesi yake ilimalizika na kurudishiwa udiwani, lakini Mbembela alipinga kwa madai kuwa Jamhuri ilimkatia rufaa hivyo anakabiliwa na kesi.

Akizungumza na gazeti hili baada ya kuapishwa juzi, Mwangonela alisema hiyo ni haki yake anayopaswa kuipata kwa kuwa uamuzi wa mahakama ulibatilisha hukumu na kumuona hana hatia, hivyo kurejeshewa udiwani na stahili zake

0 comments:

Post a Comment