Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Wednesday, September 27, 2017

Kamera za Nida zaibwa Simiyu.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) mkoani Simiyu imeibiwa kamera mbili aina ya Canon zilizokuwa zikitumika kupiga picha za vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.
Ofisa Usajili wa Nida mkoa hapa, Careen Kuwite amesema hayo leo Jumatano. Amesema kamera hizo ziliibwa wiki iliyopita na taarifa imeshawasilishwa polisi.
Kuwite amesema baada ya upelelezi kufanyika wamebaini vijana wawili wamehusika na wizi huo ambao  walikamatwa juzi.
Baada ya kukamatwa, amesema vijana hao waliwapeleka na kuwaonyesha walikozificha ambako ni uvunguni mwa kitanda.
"Mashine ya vitambulisho haiwezi kufanya kazi ya usajili bila kamera, tulikuwa na semina elekezi kwa vijana 36 wa kutusaidia kuandikisha wananchi, baada ya siku moja tulibaini upotevu huo,’’ amesema Kuwite.
Amesema baada ya kuiba kamera hizo, vijana hao walishindwa kuzitumia kwa sababu haziwezi kutumika nje ya mfumo wa Nida.
Kuwite amewataka vijana kuwa waadilifu na kutumia vizuri mali za umma bila kufanya ubadhirifu kwa sababu zinatolewa kwa manufaa ya wananchi.
Ofisa huyo amesema kamera aina ya Canon zina gharama ya Sh1.5 milioni kila moja na kwamba, watuhumiwa wako polisi na watafikishwa mahakamani baada ya utaratibu wa kisheria kukamilika.
Amesema kazi ya kuandikisha wananchi kwa ajili ya kupata vitambulisho vya Taifa imesimama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Boniventure Mushongi alipotafutwa kuzungumzia suala hilo amesema hajapata taarifa. @Mcl

0 comments:

Post a Comment