MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza kuandikisha,
kusajili na kuwatambua wananchi wa kuwapa Vitambulisho vya Taifa katika
mikoa 12 ikilenga kutoa vitambulisho hivyo kwa Watanzania wote
wanaostahili ifikapo Desemba 2018.
Akizungumza kwa simu, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew Massawe jana
aliitaja mikoa ambayo tayari imefikiwa na mamlaka hiyo kuwa ni Dodoma,
Mbeya, Njombe, Songwe, Singida, Simiyu, Geita, Mwanza, Manyara, Arusha,
Kilimanjaro na Iringa.
Pamoja na mikoa hiyo, mamlaka hiyo pia kesho inatarajia kuzindua
usajili wa wananchi kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho hivyo mkoani
Mtwara. Alisema wanashirikiana na Wakala wa Ufilisi, Usajili na Udhamini
(RITA), Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi) ili kuhakikisha kila mwananchi anayepatiwa
kitambulisho amekidhi sifa ya uraia wake.
Alisema baada ya NIDA kutoa fomu na kusajili itaingia hatua ya
utambuzi kwa kubandika majina ya wananchi waliojitokeza kujisajili ili
kutoa fursa wananchi kutambua watakaotumia fursa hiyo kujipatia
kitambulisho hicho bila kuwa na sifa.
Alisema baada ya kukamilisha utambuzi, taarifa zote zilizokusanywa
katika mikoa hiyo 12, zitawasilishwa makao makuu Dar es Salaam kutolewa
vitambulisho na mamlaka hiyo itatoa namba za utambulisho kwa wananchi
waliopitia michakato yote.
Alisema hadi kufikia Juni mwakani, wananchi wote waliopo nchini wenye
sifa na wanaostahili kupatiwa vitambulisho hivyo vya taifa watakuwa
wameshapatiwa namba ya utambulisho na ifikapo Desemba mwaka huo,
watakuwa wamepata vitambulisho.
Mkurugenzi huyo alisema, kutolewa kwa vitambulisho hivyo ni utaratibu
endelevu kwa kuwa kila mwananchi aliyefikisha umri wa miaka 18 atapata
kitambulisho hicho. Alitaja vitu ambavyo mtu anatakiwa awe navyo kukidhi
vigezo vya vitambulisho hivyo kuwa ni kuwa na cheti cha kuzaliwa na
endapo hana cheti hicho ni lazima uhamiaji imthibitishe, cheti cha
kitaaluma, kadi ya kupigia kura au hati ya kusafiria.
0 comments:
Post a Comment