Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Thursday, October 19, 2017

Ezra Chiloba wa IEBC Kenya achukua likizo ya wiki tatu.

Afisa mkuu mtendaji wa tume ya IEBC, Ezra Chiloba, ametangaza kwamba amefanya uamuzi wa kibinafsi wa kuchukua likizo ya wiki tatu kuanzia sasa, ni hivyo kutohusika katika mchakato wa uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu.

Gazeti la Daily Nation liliripoti mapema Ijumaa kwamba Chiloba alichukua uamuzi huo - siku tano tu kabla ya uchaguzi huo wa marudio uliozua utata mkubwa - kama njia ya "kurejesha imani kwa wadau ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu maafisa waandamizi wa tume hiyo."

Haya yanajiri siku mbili tu baada ya mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, kuwataka maafisa wote waliotuhumiwa kuchangia kwa dosari zilizogubika uchaguzi wa tarehe nane mwezi Agosti kujiuzulu ili kuhakikisha kuwa zoezi la marudio la tarehe 26 litakuwa la haki na ukweli.

Chiloba ni mmoja wa maafisa ambao wamekuwa wakishinikizwa kujiuzulu kabla ya mrengo wa upinzani kukubali kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio.



Mmoja wa makamishna wa tume hiyo, Roselyn Akombe, alijiuzulu siku ya Jumatano na kusema kwamba mchango wake kwenye mchakato wa uchaguzi huo haungekuwa na faida kufuatia kile alichokiita mgawanyiko mkubwa na malumbano ya mara kwa mara ndani ya tume hiyo.

Mahakama ya juu nchini Kenya ilibatilisha uchaguzi wa urais wa mwezi Agosti na kuitaka IEBC kuitisha zoezi la marudio ndani ya kipindi cha siku sitini.

IEBC ilikuwa imemtangaza rais Uhuru Kenyatta kama mshindi kwa kupata kura 8, 203, 290 dhidi ya mgombea wa NASA, Raila Odinga, ambaye aliripotiwa kupata kura 6,762,224.

Tume hiyo ilitangaza tarehe 17 kama siku ya uchaguzi huo na baadaye ikabadilisha tarehe hiyo hadi 26 mwezi Oktoba.

Punde tu baada ya uamuzi huo wa mahakama, muungano wa upinzani, NASA, ulitangaza kwamba hautashiriki kwenye uchaguzi huo wa marudio iwapo masharti 11, ambayo ulisema hayawezi kupunguzwa kamwe, hayangetimizwa na tume hiyo.

Kufikia sasa, muungano huo, ukiongozwa na Odinga, umeendelea kushikilia msimamo huo huo na kuwataka wafuasi wake kutoshiriki kwenye zoezi hilo.

Tayari Odinga ametangaza kujitoa kwa uchaguzi huo na kutaka jina lake lisijumuishwe kwenye karatasi za kura.

"Hakuna uchaguzi utakaofanyika bila mageuzi kufanyika kwenye tume hiyo.Tutafanya maandamano makubwa siku hiyo ya uchaguzi," amesema mwansiasa huyo mkongwe mara kadhaa kwenye mikutano ya kampeni na ile ya waandishi wa habari.

Hata hivyo Kenyatta, ambaye ni mgombea wa urais kwa tikiti ya chama kinachotawala cha Jubilee, ameshikilia kwamba uchaguzi huo utaendelea kama ilivyoagizwa na mahakama na kwamba hana nia ya kukutana na Odinga wala tume ya IEBC kabla ya siku ya uchaguzi.

"Mimi sina shida na IEBC...kwa nini nikutane nao?" ameuliza rais Kenyatta.

Mgawanyiko mkubwa umejidhihirisha ndani ya tume ya IEBC siku chache tu kabla ya uchaguzi huo.
@voanews

0 comments:

Post a Comment