UFAFANUZI KUHUSU MUSWADA WA
SHERIA YA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KWA WATUMISHI WA UMMA, 2017(THE
PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND ACT, 2017), KUHUSIANA NA MASUALA YA
KODI, MAFAO YA MAJAJI NA MAFAO YATAKAYOTOLEWA KWA WATEGEMEZI
Kumekuwa na tafsiri potofu kuhusu
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma
(The Public Service Social Security Fund Act, 2017), inayotolewa aidha
kwa bahati mbaya au kwa lengo la kupotosha maudhui ya Muswada huo kuwa
unakusudia kutoza kodi mafao ya Wastaafu, kubagua Wajane na kuathiri
mafao ya Majaji.
Tunapenda kuutaarifu Umma na
Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa ujumla kwamba tafsiri hiyo
siyo sahihi na ni upotoshaji mkubwa na kwa misingi hiyo tunapenda
kutoa taarifa na ufafanuzi kama ifuatavyo:
1.0. Serikali haijawahi na wala
haikusudii kutoza kodi Mafao ya Wanachama na wala si malengo ya
kifungu cha 56 cha Muswada huu. Ni vema ifahamike kwamba hata katika
Sheria za sasa za Mifuko ya Pensheni na Sheria za Kodi, mafao ya
wanachama hayatozwi kodi, rejea kifungu cha 47(3) cha Sheria ya Mfuko
PSPF, kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Mfuko wa GEPF, kifungu cha 90(2)
cha Sheria ya Mfuko wa NSSF na kifungu cha 54 cha Sheria ya Mfuko wa
PPF. Aidha, masharti na maudhui ya kifungu cha 56 cha Muswada yanafanana
kabisa na masharti ya vifungu tajwa hapo juu vikisomwa pamoja na sheria
za kodi ambazo ndiyo misingi wa misamaha yote ya kodi nchini.
2.0. Masharti kuhusu mafao ya
Majaji yamechukuliwa kutoka kwenye Sheria ya Mfuko wa PSPF ambako ni
vifungu vya 21 na 22 vya Sheria Hiyo. Hakuna mabadiliko yoyote
yaliyofanyika kwenye maudhui ya vifungu hivyo zaidi ya kuboreshwa kwa
kutenganisha masharti ya Pensheni na stahili nyingine. Hivyo taarifa
zinazotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu mafao ya Majaji ni
upotoshaji wa makusudi unaolenga kujenga taswira potofu mbele ya
macho ya Jamii.
3.0. Eneo la mafao ya Wajane na
warithi katika Muswada ni moja ya maeneo ambayo yameboreshwa kwa kiasi
kikubwa ikilinganishwa na masharti yalivyo kwenye Sheria za
sasa. Muswada umebainisha kwa uwazi stahili za Wajane na Warithi
pale mwanachama au mstaafu anapofariki.
Tunawashauri na kuwaasa wananchi
na Taasisi nyingine kuepuka kutoa maoni ambayo yanalenga kupotosha nia
njema ya Serikali katika Muswada huu.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846
Tovuti: www.ssra.go.tz
Dar es Salaam
22/1/2018
0 comments:
Post a Comment