Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe wamewatembelea
wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na
kuwashukuru Madaktari na Wauguzi kwa juhudi kubwa wanazofanya kunusuru
maisha ya watu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa anaongea na Mzee Ngosha
Miongoni
mwa wagonjwa waliojuliwa hali ni Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha)
aliyelazwa katika chumba namba 310 na Mtoto Shukuru Musa Kisonga
aliyelazwa katika chumba namba 312 ambaye hivi karibuni aliripotiwa
kuugua ugonjwa usiofahamika uliosababisha aishi kwa kunywa mafuta ya
kula, sukari na Maziwa.
Rais Magufuli na Mama Janeth Magufuli
wamefanya matembezi hayo leo majira saa moja ya asubuhi wakiwa wanatokea
katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro liliopo Oysterbay Jijini Dar
es Salaam ambako walihudhuria ibada ya Jumapili.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali
itaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali
hiyo pamoja na zile zinazowakabili madaktari na wauguzi hao.
“Jamani, Madaktari
tunawashukuru sana, mnafanya kazi nzuri, Madaktari wote nchini pokeeni
pongezi zangu, sisi serikali tutaendelea kuzikabili changamoto hizo na
siku moja zitakwisha. Kikubwa ni kumtanguliza Mungu mnapofanya kazi ya
kuokoa maisha ya watu kwa juhudi kubwa, mnafanya kazi ya Mungu” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli na Mkewe wakiwa wanaongea na Mtoto Shukuru
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru ameweza kumshukuru
Rais Mgufuli kwa kuwatembelea huku akisisitiza kuwa tayari madaktari
wamegundua magonjwa yanayomkabili Ngosha pamoja na Mtoto Shukuru.
Aidha, Prof. Museru amesema hospitali
hiyo imepiga hatua kubwa ya kujenga uwezo wa kutibu magonjwa ambayo
wagonjwa walilazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha
nyingi za serikali.
“Mhe. Rais hospitali yetu
sasa imeanza kufanya upasuaji na kutoa tiba ya magonjwa ambayo
yalilazimu wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, mfano hivi sasa tunatoa
huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa takribani 250, na kuanzia mwezi
Julai mwaka huu tutaanza kupandikiza figo.Huduma hii hugharimu kati ya
Shilingi Milioni 60 na Shilingi Milioni 70 kwa mgonjwa mmoja anayekwenda
kutibiwa nje ya nchi, lakini hapa nchini gharama zinashuka hadi
Shilingi Milioni 21” alisema Prof. Museru.
Kwa upande mwingine Prof. Museru amesema
kuwa hospitali ya Muhimbili imejipanga kuanza kutoa huduma ya matibabu
kwa watoto wenye matatizo ya usikivu ambao wapo hatarini kuwa viziwi ili
kuweza kuokoa fedha nyingi zinazokazo kwenda kuwatibu nje ya nchi,
kutoka Shilingi Mil 90 hadi Mil 30.
0 comments:
Post a Comment