Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Wednesday, June 21, 2017

86.6% ya Watanzania hawana vyeti vya kuzaliwa


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha kuwa asilimia 86.6 ya Watanzania hawajasajiliwa na hivyo hawana vyeti vya kuzaliwa.
Aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akifungua kikao cha wadau wa usanifu wa mpango wa usajili wa matukio ya binadamu. Alisema takwimu hizo zinaonesha kwamba Watanzania asilimia 13.4 ndio wamesajiliwa na wana vyeti vya kuzaliwa. “Hii ni idadi ndogo na ni kiashiria kuwa serikali haina taarifa za idadi kubwa ya wananchi,” alisema Profesa Kabudi.
Pamoja na takwimu hizo, wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila hata taarifa zao kuonekana katika kumbukumbu zozote za serikali. “Hali ya usajili wa matukio ya vifo, ndoa na talaka nayo hairidhishi pamoja na ukweli kwamba takwimu zake ni za muhimu kwa serikali,” alisema. Profesa Kabudi alisema serikali imeamua kufanya maboresho ya mfumo wa usajili uliopo kwa kuanzisha mfumo utakaofanya kazi vizuri wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu (CRVS).
“Maboresho hayo yanatekelezwa kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadam na Takwimu ambao unalenga kutatua changamoto zilizochangia hali ya usajili kutokuwa ya kuridhisha,” alisema na kuongeza: “Ni imani yangu utekelezaji wa mkakati huu utakuwa njia sahihi ya kuelekea kumuona kila mwananchi katika picha ya taifa,” alisema.
Alisema mchakato wa kurekebisha mfumo wa sheria zinazosimamia masuala ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu umeshaanza. Pia alipongeza Tume ya Kurebisha Sheria kwa kukamilisha utafiti na kufanya kwa kisayansi na kwa makini ukubwa na hivyo mwishoni mwa mwaka kutakuwa na mfumo wa kisheria uliorekebishwa. Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA, Profesa Hamis Dihenga alisema CRVS utawezesha kusajili matukio ya binadamu, lakini pia utajua sababu za vifo vinavyotokea.
Dihena alisema RITA wamekwishaanza kutekeleza maboresho ya mfumo kama mkakati wa CRVS unavyoelekeza kupitia Mpango wa Usajili wa Watoto walio na umri wa miaka mitano. “Mpango huo wa kudumu umeanza kutekelezwa katika mikoa saba na kuonesha mafanikio makubwa,” alisema.
Profesa Dihenga alisema mpango huo umewezesha kusajili watoto kwa wastani wa asilimia 77 kwa idadi ya watoto wote kwa kundi hilo kwa mikoa husika ambayo ni Njombe, Mbeya, Songwe, Iringa, Shinyanga, Simiyu na Geita. Alisema mazungumzo yanaendelea na taasisi nyingine kama NIDA, Tume ya Uchaguzi na Idara ya Takwimu Tanzania ili kuhakikisha RITA inakuwa chanzo cha kupata takwimu mbalimbali.

0 comments:

Post a Comment