Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Friday, June 30, 2017

Watafiti waja na maharage yenye faida nyingi mwilini.

IMEANDIKWA NA JOHN NDITI
MAHARAGE ni chakula muhimu na rahisi kwa Watanzania wengi linapokuja suala la mboga na pia ni chanzo cha protini kwa wengi. Kwa miaka mingi maharage yamekuwa yakilimwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, lakini katika miaka ya karibuni yamekwa yakilimwa zaidi kibiashara.
Pamoja na umuhimu wake mwilini, baadhi ya watu hawapendi kula maharage ambayo mara nyingi hutumiwa na Watanzania kama mboga kutokana na kukinai au kuyaona kama chakula cha duni au cha kimaskini.
Lakini wataalamu wa Afya wanasema maharage ni miongoni mwa mboga zenye faida kubwa mwilini na hivyo kuwa muhimu kwa watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya. Maharage, mbali ya mbegu zake kutumika kama mboga kwenye mlo wa binadamu, majani yake huweza kutumika pia kwa chakula cha mifugo.
Maharage yana viwango vingi vya protini ambavyo ni muhimu katika kujenga mwili wa binadamu na kwa msingi huo yanafaa kuwa mbadala wa nyama, maziwa, mayai au samaki. Maharage pia husaidia kukinga viwango vya sukari kwenye damu kuongezeka ghafla baada ya mlo, hivyo ni muhimu sana kwa watu wenye kisukari au wanaoelekea kupata tatizo hilo.
Wakati ukweli wa maharage ukiwa huo, watafiti wa kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian kilichopo mkoani Arusha wameibuka na aina nyingine ya mbegu za maharage zenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma na zinki kulinganisha na aina zingine za mbegu. Mtaalamu wa chakula na lishe katika kituo hicho, Mary Mdachi anasema virutubisho vilivyomo kwenye mbegu hizo mbili za maharage vinamwezesha mlaji kukabiliana na maradhi mbalimbali yanayotokana na upungufu wa protini au madini ya chuma na zinki.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya akiwa katika shamba la majaribio ya mbegu hizo, Mdachi anakiri kwamba watanzania wengi wanashindwa kumudu gharama za kununua nyama, samaki, maziwa, kuku na mayai na hivyo maharage kuwa kimbilio lao. “Ukosefu wa madini ya chuma pamoja na zinki kwa wingi kwenye mwili wa mwanadamu huchangia mtu kupata maradhi yanayosababishwa na upungufu wa damu na nguvu kwa wanaume wengi na wakiwemo vijana,” anasema Mdachi.
Anasema kituo chao kinatafiti mbegu za maharage zenye virutubisho muhimu kwa ajili ya matumizi ya binadamu ili pale mtu anapoyala aweze anufaike zaidi. Mtaalamu huyo wa chakula na lishe anafafanua kwamba madini ya chuma yanasaidia kutengeneza damu mwilini na nyuzi lishe zilizomo wenye maharage husaidia mwili kumeng’enya chakula vizuri.
Anasema kama wengi wanavyofahamu, protini inayopatikana kwa wingi katika maharage husaidia katika kujenga mwili lakini maharage hayo pia yana vitamini B ambayo inasaidia kutengeneza seli za mwili. Kwa upande zinki inasaidia sana katika kurudisha nguvu za mwili kwa wanaume, hususani suala zima la kuimarisha uzazi na kuboresha unyumba, anasema.
Anasema maharage hayo, kama yalivyo mengine, yataendelea kuwa na bei ndogo kwa kilo kulinganisha na bei ya nyama na samaki na kwamba yatawawezesha watanzania wengi kuboresha afya zao. Mtaalamu huyo anakiri kwamba watu wengi wanashindwa kula maharage kwa kuogopa gesi itokanayo na mboga hiyo na kwamba tatizo hilo linatokana na wapishi wengi kutojua mbinu bora za upikaji wa maharage.
“Nawashauri wapishi kuloweka kwanza maharage kwa usiku mmoja na ikifika asubuhi kabla ya kuyapika, maji yale yamwagwe na kuweka maji mengine na ndipo yapikwe,” anasema Mdachi. Anasema mpishi akifanya hiyo, ataondoa gesi kabisa kwenye maharage na kuwa salama kwa mlaji anayeogopa kuyala kutokana na gesi.
Mtafiti Kiongozi wa zao la maharage nchini, Papias Binangwa anasema, mbegu mpya walizozizalisha ambazo kwa sasa zipo kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Nchini (TOSCI), kwa ajili ya kuthibitishwa ubora wake ni aina ya MAC 44 na RWV 1129.
Anasema mbegu hizo tayari wamekamilisha upande wao kwa maana ya utafiti na kupeleka takwimu zote zinazotakiwa kwenye mamlaka hiyo ili nao waweze kuziangalia na kuzipitisha kama mbegu rasmi kwa ajili ya kulimwa na wakulima na hivyo kuwanufaisha walaji zaidi kulinganisha na mbegu nyingi za maharage zinazolimwa sasa.
Anaongeza kwamba, mbali na kuwanufaisha walaji, pia zina faida kubwa kwa wakulima kutokana na kuzaa kwa wingi ambapo mkulima anatarajia kupata kati ya tani 2.5 hadi 3 kwa hekta moja endapo atalima kwa kufuata maagizo ya kitaalamu. Mtafiti huyo anawashauri wakulima kuwa tayari kwa mbegu hizo pale zitakapopitishwa na mamlaka husika kwani zina faida kubwa kiafya hususani kutokana na virutubisho vingi vya madini yakiwemo ya zinki yanayoongeza nguvu za kiume.
Kituo hicho pia kimeibuka na aina nyingine tatu za mbegu za maharage yenye sifa ya usindikaji ikiwa ni mkakati wa kuwaandaa wakulima wa maharage kuwa na mbegu zinazofaa kwa ajili ya viwanda vya usindikaji maharage. Anataja mbegu hizo tatu kuwa ni SWP -9, SWP - 10 na SWP - 11 na kwamba tayari kituo kimeshakamilisha taratibu za kiutafiti na kuzipeleka kwenye taasisi ya udhibiti ubora wa mbegu TOSCI ili kuomba kibali cha kuzipitisha.
“Sio kila maharage yanayolimwa na wakulima yanafaa kusindikwa na kuuzwa kwenye maduka makubwa na madogo kwenye makopo bali kuna sifa zinazotakiwa kuonekana kwenye maharage yanayosindikwa na aina hizi za mbegu zina sifa ya usindikwaji kwa asilimia 90,” anasema Binangwa.
Anasema hii ni fursa nzuri kwa wakulima kupata faida kubwa na kwamba usindikaji wa maharage kwenye viwanda utasaidia watumiaji wa maharage kupunguza gharama za matumizi ya nishati ikiwemo kuni, mkaa, umeme na gesi kwani mtumiaji atapata maharage ambayo yameshaiva tayari.

0 comments:

Post a Comment