Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Monday, July 24, 2017

Upinzani DRC waja na mkakati mpya wa kumshinikiza Rais Kabila aondoke madarakani

Upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umetangaza mipango na mikakati yake mipya ya kushinikiza kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kwa kutumia migomo na uasi wa kiraia.
Taarifa ya wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeeleza kuwa, wapinzani wanaendelea kufanya maandamano na kuhamasisha uasi wa kiraia ili kumshinikiza Rais Kabila aachie ngazi na kuondoka madarakani.
Tangazo hilo linakuja baada ya siku mbili za mazungumzo ya upinzani jijini Kinshasa kufuatia wasiwasi kuwa Rais Kabila anayetawala taifa hilo tangu mwaka 2001 huenda akaendelea kubakia madarakani na hivyo kukiuka hata makubaliano yaliyofikiwa mwaja jana.
Uchaguzi ulitakiwa kufanyika mwaka huu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mujibu wa mkataba uliokusudia kuepusha vurugu za kisiasa nchini humo baada ya Rais Kabila kuendelea kubakia madarakani hata baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika Disemba mwaka jana.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Agosti 20 upinzani umepanga kufanya maandamano mfululizo katika mji mkuu  Kinshasa na majimbo 25. 
Mgogoro wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliibuka baada ya kuahirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais na kadhalika sisitiza la Rais Joseph Kabila la kutaka kuendelea kusalia madarakani nchini humo. Licha ya kutiwa saini makubaliano baina ya wapinzani na serikali juu ya kufanyika uchaguzi wa rais tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu, hata hivyo inaonekana kuwa, uchaguzi huo hautaweza kufanyika katika tarehe iliyopangwa.

0 comments:

Post a Comment