Mahakama ya uhalifu wa kimataifa jijini Kampala nchini Uganda, imewakuta mashehe 6 na makosa ya ugaidi kuhusiana na mauaji ya viongozi wenzao wa dini ya Kiislamu, lakini hawakukutwa na makosa ya mauaji.
Washukiwa wengine 8 katika kesi hiyo hawakupatikana na makosa yoyote, na hukumu yao inatarajiwa kutolewa siku ya Jumanne.
Sita kati yao, wakiongozwa na aliyekuwa kiongozi wa Waislam wa Tablique Sheikh Yunus Kamoga, makosa ya mauaji na jaribio la kuua yameondoshwa.
Kamoga, pamoja na mashehe wenzake 13, walikuwa wanakabiliwa na makosa ya ugaidi, mauaji na jaribio la kuua, yaliofunguliwa na mahakama miaka mitatu iliyopita.
Wote14 walishtakiwa kwa makosa ya kuwaua mashehe Mustapha Bahiga, Abdu Kadhir Muwaya, Hassan Kirya kwa kutumia bunduki, na kujaribu kumuua Sheikh Harunah Jemba, miaka 3 iliyopita.
Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Ezekiel Muhangazi, Jumatatu wamekubaliana kwamba sheikh kamoga na wenzake watano, wako hatiani sio kwamba kuna ushahidi wa kutosha mbele ya mahakama, lakini kwa sababu ya mazingira waliopatikana nayo, yaliyowahusisha na vifo hivyo, pamoja na matamshi yao, yaliyotolewa kama vitisho kabla ya mauaji kutokea.
“Waislamu hawajahi kujihusisha na visa vya mauaji. Hii leo mahakama imethibitishwa usemi wetu wa kila siku. Ushahidi ambao umetumika kuwaondolea mashtaka ndio ushahidi ambao umetumika kuwatia hatiani. Kama viongozi wa Waislamu tuna furaha licha ya kuwa wengi wa Waislamu wana huzuni,” amesema mmoja wa viongozi wa Waislam wa Tabliq
Kwa mujibu wa mahakama washukiwa wengine 8 hawana hatia, na wataachiliwa huru. Nao ni Amir Kinene, na nduguye Hakeem Kinene, Sematimba Abdul Rashid, Hamza Kasirye, Sekitto Twaha, Jingo Rashid, Musa Isa Mubiru na Yiga George William.
Mahakama inatarajiwa kutoa maamuzi ya mwisho siku ya Jumanne.
Kesi hii imekumbwa na changamoto chungu nzima, zikiwemo kuuawa kwa aliyekuwa msimamizi wa mashtaka Joan Kagezi.
Hata hivyo waandishi wa habari walipewa masharti ya kutopiga picha majaji, wala kutaja majina yao. Kutohoji familia za washukiwa wala kukaribia washukiwa, miongoni mwa masharti mengine.
Wengi wa waliotoa ushahidi mahakamani walifichwa na waliofuatilia waliweza tu kusikia sauti iliyoharibiwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Yote hayo yalikuwa ni kwa sababu ya hofu ya kushambuliwa.
Usalama uliimarishwa nje na ndani ya mahakama, mda wote kesi ilipokuwa ikiendelea kwa mda wa miaka 3.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda.
0 comments:
Post a Comment