Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Thursday, September 28, 2017

WAKAZI 120,000 WAPYA HUSAJILIWA KILA MWAKA JIJINI DAR.

JIJI la Dar es Salaam ni miongoni mwa miji mikubwa nchini inayoathiriwa na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Ili kukabiliana na tatizo hilo Tanzania inahitaji dola za Marekani milioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri miji mikubwa likiwamo jiji la Dar es salaam.
 

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa kimataifa unaojadili kuhusu makazi, uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi ulioandaliwa na Chama cha Wataalamu na Wadau wa Mazingira Duniani (IAPS) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Ardhi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya, ipo haja ya wataalamu wakatafuta suluhu ya matatizo hayo.

“Kwa sasa Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la watu 120,000 kila mwaka, tatizo ambalo linakwenda sambamba na tatizo la makazi, maji safi na salama, usafi wa mazingira na tatizo la ajira,” alieleza Samia.


Katika Mkutano huo wa kwanza kufanyika nchini na unahudhuriwa na nchi wanachama 16 kutoka mabara manne Makamu wa Rais aliwataka Chuo Kikuu Ardhi kwa kushirikiana na wataalamu wengine kwenye mkutano huo, kuja na maazimio na mapendekezo yatakayoisaidia nchi kutatua tatizo la mipango miji, makazi holela, miundombinu, utawala na usimamizi wa mazingira ili kufikia ajenda ya ukuaji miji ya mwaka 2030.


Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Evaristo Liwa alisema uharibifu wa mazingira kwa Jiji la Dar es Salaam ni mkubwa kutokana na ujenzi holela, uchimbaji wa mchanga, kuziba mifereji ya maji na uharibifu wa kingo za bahari.

Profesa Liwa alisema wajibu wa kwanza wa kutunza miji na mazingira ni wa jamii yenyewe na serikali kupitia Sera ya Mipango Miji ihakikishe wananchi wanajenga kwenye maeneo yaliyopangwa na kuboresha maeneo ambayo yamejengwa kiholela.

Kwa upande wake, Dk Nathalie Jean-Baptiste kutoka IAPS ambao ni waandaaji wa mkutano huo, alieleza kuwa chama hicho kina jumla ya wanachama 400 duniani kote.

Alisema wajumbe katika mkutano huo watajadili mifano hai kutoka baadhi ya miji kama Dar es Salaam na Mwanza ambayo pia imeathirika kutokana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, lakini pia mapendekezo yatakayotolewa kwenye mkutano huo yatasaidia kupambana na matatizo ya mafuriko, makazi holela na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi mijini.@TSN.

0 comments:

Post a Comment