Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Tuesday, October 3, 2017

BAADA YA VIKWAZO BURUNDI YAANZA KUJITEGEMEA KIBAJETI


SERIKALI ya Burundi, kuanzia mwaka 2018 itaanza kujitegemea kibajeti kwa asilimia 100.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Domitien Ndihokubwayo alipokuwa anazungumza na wakuu wa idara na wafanyakazi wa wizara hiyo mjini Ngozi hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine, walikutana kujadili sera na usimamizi wa kodi ili kuweka mikakati ya kuibua vyanzo zaidi vya mapato.
“Tunatakiwa kukusanya mapato kadiri inavyowezekana kwa sababu lengo la serikali ni kujitegema kibajeti kwa asilimia 100 na makusanyo hayo lazima yatokane na vyanzo vya ndani, badala ya asilimia 70.3 ya sasa,” alisema. Mwaka 2017, Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR) imepanga kukusanya Faranga za Burundi bilioni 720 ambazo zitachangia asilimia 70 katika bajeti ya serikali iliyopanga kutumia Faranga trilioni 1.3.
Naye Faustin Ndikumana, Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Maneno na Vitendo katika Mabadiliko (PARCEM), anasema Serikali ya Burundi inapaswa kuainisha matumizi yenye manufaa kwa taifa. Aidha, ameshauri serikali ifikirie kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa lengo la kuliingizia taifa fedha za kigeni zitakazosaidia kuboresha maisha ya Warundi. “Mahitaji yote ya Warundi hayawezi kutekelezwa kwa fedha za ndani.
Hakuna nchi duniani inayojitosheleza kwa kila kitu, lazima waingize fedha kwa kuuza bidhaa nje ya nchi yao,” alisema Ndikumana. Machi mwaka 2016, Jumuiya ya Ulaya (EU) iliyokuwa inaisaidia sana Burundi ilitangaza kuacha kuisaidia nchi hiyo kibajeti, kama moja ya masharti ya kuitaka itafute suluhu ya migogoro ya kisiasa iliyosababisha machafuko na mauaji.

0 comments:

Post a Comment