Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Monday, October 30, 2017

Raia kumi wa Iran na watanzania wawili wapandishwa kizimbani kwa tuhuma za madawa ya kulevya

 Raia 10 wa Iran na Watanzania wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kusafirisha dawa za kulevya zikiwemo kilo 111.02 za heroin.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa akiwasomea mashtaka leo Jumatatu Oktoba 30,2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa amedai walikamatwa katika Ukanda wa Bahari ya Hindi upande wa Tanzania.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 25,2017. Pia, wanadaiwa walikutwa wakisafirisha gramu 235.78 za bangi.

Mbali ya hayo, Mutalemwa amedai washtakiwa walisafirisha mchanganyiko wa dawa za kulevya za bangi na kuberi zenye uzito wa kilo 3.34.

Mashtaka hayo yalisomwa kwa Kiswahili na baadaye kutafsiriwa kwa Kiirani na mkalimani Meja Ndakeye (45).

Washtakiwa hawakuruhusiwa kuzungumza chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo bali Mahakama Kuu.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika na washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Novemba 13,2017 itakapotajwa.

Kutokana na kiwango cha dawa hizo kuwa kikubwa, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuwapatia dhamana washtakiwa.

Washtakiwa hao ni raia wa Iran, Nabibakshsh Bibarde, Mohammed Dorzade, Abdallah Sahib, Ubeidulla Abdi, Naim Ishaqa, Moslem Amiree, Rashid Badfar, Omary Ayoub, Tahir Mubarak na Abdulmajid Asqan. Watanzania ni Ally Abdallah na Juma Juma.

0 comments:

Post a Comment