Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

Labels

Monday, October 9, 2017

Watu 37 waliuawa wakati wa ghasia za uchaguzi Kenya.

Tume ya taifa ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya, KHCHR, imedai kuwa jeshi la polisi nchini humo liliwaua watu 35 wakati wa ghasia zilizozuka wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.

Idadi hiyo ni ya juu kuliko ilivyoripotiwa na mashirika mengine ya haki za kibinadamu.

Mwishoni mwa mwezi Agosti, shirika Human Rights Watch lilisema watu 12 waliuawa na wengine 100 kujeruhiwa polisi walipokuwa wakikabiliana na waandamanaji maeneo ya magharibi mwa Kenya. Shirika hilo halikutoa idadi ya waliofariki jijini Nairobi na miji mingine wakati huo.



KNHCR imesema ni watu wawili pekee kati ya 37 waliofariki wakati huo ambao hawakuuawa na polisi.

Ikizindua ripoti kuhusu uchaguzi huo Jumatatu jijini Nairobi, KNCHR imesema kuwa polisi pia walitumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na waandamanji wa mrengo wa upinzani National Super Alliance (Nasa) walipokuwa wakiwatawanya.

Makabiliano makali kati ya waandamanaji wa upinzani na polisi yalizuka kati ya tarehe 9 na 15 mwezi Agosti baada ya tume huru inayosimamia uchaguzi nchini, IEBC, kumtangaza Rais wa sasa Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais.

Mgombea wa Nasa, waziri mkuu wa zamani Raila Odinga alimaliza wa pili katika uchaguzi huo kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na IEBC.

KNCHR inadai kuwa visa 123 kati ya 126 vya watu kuumizwa vibaya msimu huo aidha viliwahusisha maafisa wa polisi kuwapiga waandamanaji na watu kwenye nyumba zao wakati wakishika doria haswa katika mitaa ya mabanda katika miji, sana jijini Nairobi na Kisumu.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa baada ya kufuatilia uchaguzi pia inanakiri kuwepo na uvunjaji wa sheria za uchaguzi na wanasiasa waliokuwa wakiwania nyadhifa mbalimbali.

KNCHR inadai kuwa kando na kuwepo visa vya utoaji hongo kwa wapiga kura kulitokea pia usafirishaji wa wapiga kura kuelekea maeneo fulani na kuwepo kwa vifaa vya kampeni katika vituo vya kupigia kura kinyume na sheria.

Mwenyekiti wa tume hiyo Kagwiria Mbogori akizungumza na BBC hata hivyo amesema kuwa kuna haja ya tume ya uchaguzi IEBC kujipanga sawasawa na kufanya marudio ya kura za urais kama ilivyoamrishwa mahakama kuu ili kuzuia hali ya suitafahamu ambayo inazidi kulemaza uchumi wa taifa.

Mahakama kuu nchini humo ilibatilisha ushindi wa Rais Kenyatta mapema mwezi Septemba baada ya upinzani kwenda kotini wakidai kuwa uchaguzi ulikumbwa na ukiukaji wa sheria za uchaguzi na hivyo basi kufanya vigumu kubaini mshindi kamili wa uchaguzi huo.


Upinzani ulidai mitambo ya teknolojia ya IEBC ilidukuliwa na matokeo kuingiliwa kumfaa Bw Kenyatta. @bbcswahili

0 comments:

Post a Comment