Rais John Magufuli ametengua 
uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ya Wilaya ya Tunduru,
 Abdallah Mussa kwa kushindwa kumudu majukumu yake.
 
Kutenguliwa
 kwa uteuzi wa mkurugenzi huyo leo Alhamisi Novemba 9,2017 kumefanyika 
siku tatu baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa wakurugenzi wengine 
wawili.
Taarifa ya Rebecca Kwandu, mkuu wa kitengo cha 
mawasiliano serikalini katika ofisi ya Tamisemi imesema Katibu Mkuu 
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mussa Iyombe ndiye 
aliyotoa taarifa ya kutenguliwa kwa uteuzi huo leo mjini Dodoma.
Amesema kutokana na hatua hiyo, uteuzi wa mkurugenzi mwingine utafanyika baadaye.
Rais
 Magufuli Novemba 6,2017 alitengua uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri 
za Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa Halmashauri ya Bukoba, 
Mwamtumu Dau.
Viongozi hao walishindwa kutaja kiasi cha
 fedha za Mfuko wa Barabara zilizopokewa kwenye halmashauri zao 
walipoulizwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa 
Bukoba.
Alipoitwa mbele na kutakiwa kutaja kiasi halisi
 cha fedha zilizopokewa katika halmashauri kwa ajili ya mfuko huo, 
Mwantumu alijibu kuwa ana idara nyingi anazozisimamia hivyo isingekuwa 
rahisi kwake kukumbuka kila kitu, hivyo ni mpaka awepo mweka hazina. 
Pia, alisema hawezi kusema uongo.
Dk Magufuli katika mkutano huo alisema amewasamehe lakini baadaye Ikulu ilitoa taarifa ikieleza Rais ametengua uteuzi wao.
 
 
 
0 comments:
Post a Comment