Rais John Magufuli ameanza ziara 
rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Uganda kwa mwaliko wa Rais 
Yoweri Museveni.
Dk Magufuli aliyeongozana na mkewe 
Janeth amewasili Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ambako amepokewa
 na mwenyeji wake Rais Museveni aliyeambatana na mkewe Janeth.
Katika
 mapokezi hayo leo Alhamisi Novemba 9,2017, Rais  Magufuli amepigiwa 
mizinga 21 na amekagua gwaride  lililoandaliwa kwa heshima yake.
Wakiwa mpakani, viongozi hao wawili watafungua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post - OSBP) kilichojengwa ili kurahisisha utaratibu wa forodha, uhamiaji na kuharakisha biashara kati ya nchini hizi mbili.
Taarifa
 ya Ikulu imesema baadaye leo, marais hao wataweka jiwe la msingi katika
 mradi wa bomba la mafuta ghafi linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi 
Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Shughuli hiyo itafanyika katika Kijiji cha Luzinga, kilichopo mkoani Rakai nchini Uganda.
Baada
 ya ufunguzi, viongozi hao watazungumza na wananchi katika mkutano wa 
hadhara utakaofanyika  wilayani Kyotera nchini Uganda.
Rais Magufuli jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais Museveni katika mji wa Masaka. @MCL.
 
 
 
0 comments:
Post a Comment