Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi mpya
wa Uganda nchini Mhe. Richard T. Kabonero aliyefika ofisini kwa Makamu
wa Rais kujitambulisha na kufanya mazungumzo, Ikulu jijini Dar es
salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya
pamoja Balozi mpya wa Uganda nchini Mhe. Richard T. Kabonero mara baada
ya kumaliza mazungumzo, Ikulu jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya
Makamu wa Rais)
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akimkaribisha ofisini kwake Balozi wa Cuba nchini Mhe. Lucas Domingo
Hernandez . (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akisalimiana na Balozi wa Iran nchini Mhe. Moussa Farhang aliyefika
ofisini kwa Makamu wa Rais kwa mazungumzo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa
Rais).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia kitabu chenye
historia ya miji ya Iran ambacho alikabidhiwa na Balozi wa Iran nchini
Mhe. Moussa Farhang aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kwa mazungumzo.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
…………………………………………………………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amekutana na Mabalozi kutoka
nchi tatu kwa wakati tofauti ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais alianza kwa
kukutana na Balozi Mpya wa Uganda hapa nchini Mhe. Richard T. Kabonero
ambaye alifika kuonana na Makamu wa Rais kwa mara ya kwanza ambapo
alitumia nafasi hiyo kujitambulisha.
Katika mazungumzo na Makamu wa
Rais, Balozi Kabonero alizungumzia nia ni ya dhati ya nchi yake katika
kudumisha na kuimarisha uhusiano wa kindugu baina ya Tanzania na Uganda
hasa ushirikiano wa kijamii, na kiuchumi ambapo tafiti za mafuta
zinazoendelea katika ziwa Eyasi, mashirikiano ya sekta ya anga ili
kusaidia kukuza utalii, mradi wa ujenzi ya reli ya kati na mradi wa
umeme vijijini pamoja na kuanzishwa kwa jukwaa la biashara la sekta
binafsi kutoka nchi husika ili kuweza kunufaika na fursa
zitakazojitokeza baada ya kukamilika bomba la mafuta .
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Uganda kwa kutimiza miaka 55 ya Uhuru.
Pia aliipongeza Uganda kwa
kutafiti na kugundua mafuta kwa kutumia wataalamu wazawa ambapo
alisisitiza ushirikiano wa kitaalamu na wataalamu wa Tanzania.
Makamu wa Rais amemtakia heri na
fanaka katika majukumu mapya ya Ubalozi wa Uganda hapa Tanzania na
kumhakikishia ushirikiano wa Serikali.
Makamu wa Rais alimalizia
mazungumzo yake na Balozi huyo wa Uganda hapa nchini kwa kutoa shukrani
zake za dhati kwa Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa ushirikiano
wake walioutoa wakati wa ajali mbaya ya gari iliyowakuta Watanzania
waliokuwa wanatoka Harusini ambapo watanzania 13 walifariki.
Wakati huohuo Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekutana
na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Lucas
Hernandez ambaye alisema Cuba imeendelea kuwa rafiki mzuri wa Tanzania
na kushukuru sana Tanzania kuisemea Cuba iondolewe vikwazo kwenye
mkutano wa 72 wa baraza kuu la usalama la umoja wa Mataifa.
Balozi huyo alisema kuna zaidi ya
wataalamu 50 kutoka Cuba wapo nchini katika kusaidia katika Nyanja
mbalimbali ikiwemo afya na elimu,
Balozi Hernandez alisema wataalam 16 wa masuala ya afya waliwasili jana na kupangiwa kazi katika hospitali ya Muhimbili.
Cuba na Tanzania zimeendelea kuimarisha na kudumisha uhusiano uliohasisiwa na Fidel Castro na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alisema mwisho wa mwezi huu
kutakuwa na maonyesho ya biashara nchini Cuba ambapo Tanzania
itawakilishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara na Ujumbe wake.
Kwa upande wake Makamu wa Rais
alishukuru Balozi wa Cuba kufika na kumuona na kwamba anatambua
uhusiano mzuri uliopo katika nchi hizi mbili ambapo Tanzania imeendelea
kufaidika na misaada ya kitaalamu kutoka Cuba haswa katika kutupatia
wataalamu wa masuala ya afya, elimu ambapo pia Makamu wa Rais aliitaka
Cuba kuja kutangaza vyuo vyao vya elimu ya juu kwani elimu yao haina
gharama.
Makamu wa Rais aliishukuru Cuba kwa kuweza kusaidia ujenzi wa Viuatilifu kwa kuzuia malaria nchini.
Katika kukuza utalii Makamu wa
Rais alisema nchi hizi zinaweza kuimarisha mahusiano ya kitalii kwa
kupeana ujuzi mbali mbali ambapo Cuba ni wazuri kwa Utalii wa Ufukweni.
Makamu wa Rais alisema kufunguliwa kwa Ubalozi itakuwa chachu katika kuimarisha na kudumisha uhusiano.
Mwisho Makamu wa Rais alimalizia
mazungumzo na Balozi wa Cuba kwa kumpongeza Rais wa Cuba Mhe. Raul
Castro kwa kusimamia maono na misingi iliyoachwa na Fidel Castro.
Mwisho Makamu wa Rais alikutana
na Balozi wa Iran nchini Mhe. Moussa Farhang ambaye alifikisha salaam
zake kutoka kwa Makamu wa Rais wa Iran ambaye ameshukuru kwa mahusiano
yaliodumu kwa miaka 40 .
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia
alisema uhusiano uliopo baina ya nchi mbili hizi umegawanyika sehemu
mbili ambapo moja ni uhusiano wa Kiserikali na pili ni husuniano wa
kindugu ambapo mpaka leo kuna baadhi ya Vijiji, Makaburi na Misikiti
inayoonyesha kuwa wa Persia waliishi Zanzibar.
Uhusiano wa Kiserikali umeendelea
kuwa mkubwa katika Nyanja za kilimo na afya pamoja na kuendeleza
baadhi ya programu katia vyuo vya ufundi.
Makamu wa rais alisema Tanzania
inaangalia namna ambavyo itarahisisha kurejesha vikao vya tume ya pamoja
ya makubaliano ili kuweza kusukuma mbele maendeleo ya viwanda, Gesi na
biashara.
0 comments:
Post a Comment