Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Chadema), Pamela Massay
ameamua kujitolea kusukuma katika bunge hilo hoja ya mtoto wa kike
anayejifungua wakati anasoma katika shule za msingi na sekondari aweze
kuendelea na masomo yake.
Pamela anaona kwamba iwapo
ataiwasilisha hoja hiyo katika chombo hicho cha kutunga sheria cha nchi
za Afrika Mashariki na ikapita, itasaidia kumaliza mjadala baina ya wale
wanaopinga mtoto huyo asiruhusiwe kuendelea na wanaoiunga mkono.
Hoja
hiyo ambayo imekuwa ikiibuka na kupoa, hivi karibuni ilisababisha
mjadala uliochukua muda mrefu lakini baadaye ulifungwa na msimamo wa
Rais John Magufuli.
Hata hivyo, Juni 22 akiwa ziarani
mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema katika uongozi wake hakuna mtoto wa
kike atakayebeba mimba akiwa shuleni ambaye ataruhusiwa kurejea
kuendelea na masomo.
Hata baada ya kauli ya Rais baadhi
ya asasi za kiraia na mashirika yanayotetea masuala ya jinsia na haki
za binadamu yaliendelea kutoa mapendekezo mbalimbali lakini msimamo wa
Serikali haukulegezwa.
Katika hafla fupi ya maadhimisho
ya siku ya mtoto wa kike duniani iliyoandaliwa na Taasisi ya Health
Promotion Tanzania jana, Pamela alisema kama kijana aliyepitia
changamoto nyingi akiwa mwanafunzi, atahakikisha suala hilo linafika
katika Bunge la Afrika Mashariki ili liundiwe mapendekezo ya kikanda.
“Kuzuia
watoto kurudi shule baada ya kujifungua ni lazima kwanza uhakikishe
umewaondolea vikwazo vyote vinavyosababisha mimba hizo, bila kutatua
changamoto za kimazingira zinazowakabili na kuwapatia elimu ya kutosha
ukiwazuia ni kutowatendea haki,” alisema.
Mbunge huyo
alisisitiza kuwa pindi bunge litakapoanza vikao vyake atatumia kamati ya
jinsia na vijana kuhamasisha kujadiliwa kwa hoja hiyo kwa ajili ya
kupata mwafaka kwa Watanzania na wana jumuiya kwa ujumla.
Kwa
upande wake, meneja wa mradi wa utetezi wa Health Promotion, Greysmo
Mutashobya alisema takwimu zinaonyesha asilimia 18 ya Watanzania ni
watoto wa kike wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 19 hivyo kundi hilo
linatakiwa kupata huduma bora ya elimu.
“Serikali
inapaswa kutengeneza mazingira ya usawa ambayo yataweza kuhamasisha
elimu kwa mtoto wa kike sanjari na kuondoa vizuizi vilivyoko mbele yake
katika kuipata elimu hiyo,” alisema Mutashobya. @MCL
0 comments:
Post a Comment