Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani



Kwa habari za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiburudani

HABARI KWA WAKATI KUTOKA HAPA

Tunakuhakikishia kupata habari zote zilizo muhimu kutoka ulimwenguni kote kwa wakati, unaweza kusubscribe mtandao wetu na ukawa unapokea habari zote katika email yako punde tu tuchapishapo machapisho yetu. Jiunge na mitandao yetu ya Facebook na Twitter kutupata kirahisi.

HABARI ZA MICHEZO

Sasa African news tunakuhakikishia kupata taarifa zote za kimichezo kutoka viwanja mbalimbali duniani, lengo ni kuhakikisha hupitwi na lolote katika ulimwengu wa michezo.Jiunge na mitandao yetu ya Facebook na Twitter kutupata kirahisi.

TAARIFA ZA BURUDANI NA HABARI ZA WASANII

Unapenda masuala ya burudani? Ni jukumu letu kuhakikisha unazipata info zote za burudani na wasanii wanaokupa burudani, unapata video mpya, movie pamoja na muziki. Kaa karibu nasi.

KURASA ZA MAGAZETI KILA SIKU

Tunakupatia kila ambacho kinaandikwa katika magazeti ya Tanzania na nje ya Tanzania, usitie shaka ukishindwa kununua gazeti uipendalo, sogea karibu nasi na upate kila unachokihitaji.

MAHUSIANO

Fahamu mambo mengi katika ulimwengu wa mapenzi kwa kupitia dondoo, simulizi na visa mbalimbali kupitia Jim Media Online, Jiunge na mitandao yetu ya Facebook na Twitter kutupata kirahisi.

Labels

Tuesday, January 23, 2018

KAMPENI ZA UBUNGE JIMBO LA SIHA CHAMA CHA MAPINDUZI CHASISITIZA KUICHAGUA CCM NI KUCHAGUA MAENDELEO


IMG-20180122-WA0145
22 Januari 2018, 
Katika kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Siha Kata ya Ngarenairobi, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole, amewaeleza wananchi wa Jimbo la Siha kuwa kuichagua CCM ni kuchagua maendeleo ya watu wa Jimbo la Siha.
Kampeni za kumnadi mgombea Ubunge wa CCM, zimehudhuriwa na umati wa wananchi wa wilaya ya Siha na Viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Patrick Peter Boisafi.
Katibu Mwenezi wa CCM amewaeleza wananchi, CCM inazifahamu changamoto za Jimbo la Siha ikiwa ni pamoja na suala la Ardhi, Huduma za afya na Suala la Shule ya Msingi na Sekondari. Hivyo  CCM ipo tayari kuzitatua changamoto hizo kwa wakati baada ya timu ya kuleta maendeleo kukamilika endapo wananchi wa Jimbo la Siha watamchagua kwa kura nyingi Dr Godwin Mollel kuwa Mbunge wa Siha kwa tiketi ya CCM.
IMG-20180122-WA0146
*Baada ya Dr. Mollel kutazama na kuona maendeleo yanacheleweshwa na Chama chake cha awali (Chadema) ambacho hakina dira wala muelekeo, Dr Mollel ameamua kujumuika na timu ya ushindi, waheshimiwa wananchi mchagueni Dr Mollel awatumikie ,awahudumie na awaletee maendeleo. Lazima ifike wakati tunapomtafuta mwakilishi ambaye anakwenda kuwawakilisha wananchi, tupate mwakilishi ambaye akiwatazama usoni anajua shida na changamoto zenu*. Amesema Ndg. Polepole.
Katika mkutano huo wananchi wameelezwa  juu ya tabia za vyama vya upinzani kukosa msimamo katika kusimamia agenda za wananchi na kuwasihi kutovichagua vyama hivyo. *Chama kisicho kuwa na msimamo hakipaswi kupewa dhamana yoyote ya uongozi. Walisema hatuna shirika la ndege, walisema kuhusu baadhi ya watu ni mafisadi, walisema Rais asisafiri kwenda nje ya nchi, walisema kuhusu madini na sasa tunaye Ndg. Magufuli anayechukizwa na rushwa na kila aina ya ubadhirifu wa mali za umma, anatenda sawasawa na matakwa ya wananchi wa Tanzania lakini wapinzani sasa wanasema kinyume na kupinga kila jema*. Amesisitiza Ndg. Polepole.
Huu ni muendelezo wa ziara za Katibu Mwenezi wa CCM zenye lengo la kujenga Chama pamoja na kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2015- 2020.
Imetolewa na,   
*IDARA YA ITIKADI NA UENEZI*
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
SIHA, KILIMANJARO

'Dawa ya Ukimwi karibu iniue'

Yahya Jammeh administering his herbal anti-HIV paste in 2007Kiongozi wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh ambaye aliondoka madarakani na kuihama nchi hiyo mwaka uliopita baada ya kutawala kwa miongo miwili ametuhumiwa kutenda makosa mengi.

Lakini moja ya makosa hayo ni jambo la kushangaza - kuwalazimu maelfu ya watu waliokuwa na virusi vinavyosababisha Ukimwi kunywa dawa yuke ambayo alidai kuivumbua.

Dawa hiyo ilikuwa mchanganyiko wa mitishamba.

Mwandishi wetu Colin Freeman anasema watu kadha walitafiki baada ya kutumia tiba hiyo kutoka kwa Bw Jammeh.

Lamin Ceesay, mtu wa kwanza kutangaza hadharani kwamba alikuwa na virusi vya Ukimwi nchini Gambia, alifikiria kwamba alikuwa anafanya jambo la busara sana.

Ilikuwa mwaka wa 2000, na ufahamu kuhusu Ukimwi Afrika bado haukuwa pevu, na waliokuwa na virusi hivyo walikabiliwa na unyanyapaa na kubaguliwa sana katika jamii.

Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huo, Ceesay alijipatia ujasiri na kutangaza hadharani kwamba alikuwa na Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU).

Alishiriki pia matembezi ya kuhamaisha watu kuhusu virusi hivyo, ambayo yaliandaliwa na shirika moja la hisani.

Hatua hiyo ilimpa umaarufu na kumfanya kuheshimiwa na wahamasishaji wa jamii kuhusu Ukimwi duniani.

Lakini miaka michache baadaye, aliangaziwa na Rais wa Gambia Yahya Jammeh. 

Ilikuwa ni mapema mwaka 2007, Jammeh alipotangaza kwamba alikuwa amevumbua tiba ya ajabu ya virusi hivyo, ilikuwa ni mchanganyiko wa dawa za mitishamba na mbinu nyingine za kiroho za kuwatibu wagonjwa.

Jambo lililoshangaza hata zaidi ni kwamba Jammeh alisema tiba hiyo ilifanya kazi Alhamisi na Jumatatu pekee.

Si ajabu kwamba hatua ya Jammeh ilishutumiwa vikali na wakuu wa afya duniani.

Lakini nchini Gambia kwenyewe, kumwambia rais kwamba alikuwa anahubiri upuzi lilikuwa jambo ambalo hungethubutu, ungejipata jela.

Kwa hivyo, shirika la Ukimwi alilokuwa anafanyia kazi Ceesay lilipopokea barua, ikiomba watu 10 wajitolee kwenda kufanyia majaribio dawa hiyo ya rais kwa miezi sita, aliamua hangeachwa nyuma.
  Lamin Ceesay 
Lamin Ceesay alilazimishwa kuacha kutumia dawa zake za kupunguza makali ya VVU  

"Nilifikiria kwamba kuhusu kuwatuma watu wengine tu kwa mpango huo, lakini nilihofia kwamba iwapo zingeenda nami pia, ningekuwa matatani," aliniambia.

"Nilifikiria, 'Mbona nisiende? Haiwezi kunidhuru'."

Lakini Ceesay alikuwa amenoa.

Ilikuwa ni hadi alipofika katika kliniki ya muda ya rais katika ikulu ambapo walifafanuliwa sheria za mpango huo.

Hakuna uvutaji sigara, au kunywa chai au kahawa.

Hakuna kushiriki ngono.
Na muhimu zaidi, hakuna kunywa dawa za kuundiwa viwandani - ikiwa ni pamoja na dawa za kupunguza makali ya Ukimwi ambazo zilikuwa zinatolewa na madaktari.

Hangerudi nyuma tena, hata hivyo.

Walinzi wa Jammeh wakiwa na silaha walikuwa wanalinda lango la kliniki hiyo usiku na mchana.
Kwa miezi sita iliyofuata, walisema, hakuna mgonjwa ambaye angeruhusiwa kuondoka bila idhini ya Jammeh.

Na hapo basi, tiba ikaanza.

Kila siku asubuhi, rais angefika na kuwapaka dawa iliyofanana na mafuta mwilini, huku akisema sala kutoka kwa Koran ambayo ilikuwa na jalada la ngozi.

Kisha, mara mbili kwa siku, walilazimishwa kunywa mchanganyiko wa mitishamba wa rangi ya manjano kutoka kwenye chupa.

Jammeh alikataa kusema dawa hiyo ilikuwa na nini, licha yake kuambiwa kwamba iwapo Jammeh alikuwa amevumbua tiba ya Ukimwi basi Gambia ingekuwa tajiri ghafla.

Dawa hiyo ilimfanya Ceesay kuhara sana.

Aidha, aliambukiwa kifuakikuu na wagonjwa wengine, na mwishowe akadhoofika kiafya kiasi kwamba ililazimu kurejeshwa hospitali ya kawaida.

Baada ya kupimwa, ilibainika kwamba kiwango chake cha virusi mwilini kilikuwa kimepanda sana, na akaanza kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo tena.

Ceesay alikuwa miongoni mwa waliokuwa na bahati.

Mkewe, ambaye alikuwa anaugua Ukimwi pia, alifariki akipokea tiba hiyo ya rais, sawa na wagonjwa wengine wengi waliokuwa pamoja naye.

"Kama mtu mashuhuri miongoni mwa waliokuwa na Ukimwi, nilikuwa nahudhuria mazishi kila wakati," anasema.

Hali hiyo, hata hivyo, ilikuwa tofauti sana na aliyojaribu kuionesha Rais Jammeh ambaye aliwalazimisha wagonjwa kutokea kwenye televisheni kusifu ufanisi wa mpango huo.

Miongoni mwao alikuwa Ousman Sowe, aliyekuwa na shahada ya kwanza katika afya ya umma kutoka kwa chuo kikuu cha Leeds, Uingereza.

Jammeh, katika juhudi za kuupa mpango wako usomi kiasi, alikuwa amemwita Sowe na kumteua kuwa msemaji wake, kujaribu kuwapuuzilia mbali wanahabari wa kigeni waliokuwa na maswali chungu nzima.

Wakati mmoja, Sowe aliambia mwanahabari wa BBC kwamba alikuwa na "imani 100%" kuhusu tiba hiyo.

Ukweli ni kwamba, kutotumia dawa za kupunguza makali ya VVU kulimfanya kudhoofika kiasi kwamba hangeweza kupanda ngazi kwenye majumba.

"Kama mtu aliyekuwa amesoma, nilijua ulikuwa upuuzi," anakumbuka Sowe.
"Lakini singesema chochote dhidi ya mpango huo, ingawa watu walikuwa wanafariki dunia."

Sowe na wagonjwa wenzake walionusurika sasa wanafanya kazi na shirika la Aids-Free World kutoka Marekani ambalo linataka Jammeh ashtakiwe kutokana na mpango huo.

Shirika hilo linasema huo ndio pengine moja ya ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu ambao ulitekelezwa na utawala wa Jammeh.

La kusikitisha zaidi ni kwamba tofauti na magereza ya kisiri na vyumba vya mateso, ni mpango ambao uliendeshwa ulimwengu wote ukitazama.

Jammeh hakuwa na wasiwasi kuhusu hilo hata hivyo.

Afisa wa ngazi ya juu ya Umoja wa Mataifa aliyeupinga mpango huo alifukuzwa nchini Gambia.
Inaaminika kwamba jumla ya watu 9,000 walipokea tiba hiyo.

Kwa kuwa Jammeh aliweka siri nyaraka za mpango huo, hakuna mtu yeyote ambaye amebaini idadi kamili ya waliofariki.

Jambo moja ni wazi hata hivyo - kwamba mwujiza pekee kuhusu tiba hiyo ni kwamba kuna watu walinusurika.

Picha na Colin Freeman-BBC





Monday, January 22, 2018

Taarifa kwa Umma kutoka Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)

index
UFAFANUZI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KWA WATUMISHI WA UMMA, 2017(THE PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND ACT, 2017), KUHUSIANA NA MASUALA YA KODI, MAFAO YA MAJAJI NA MAFAO YATAKAYOTOLEWA KWA WATEGEMEZI
Kumekuwa na tafsiri potofu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (The Public Service Social Security Fund Act, 2017), inayotolewa aidha kwa bahati mbaya au kwa lengo la kupotosha maudhui ya Muswada huo kuwa unakusudia kutoza kodi mafao ya Wastaafu, kubagua Wajane na kuathiri mafao ya Majaji.
Tunapenda kuutaarifu Umma na Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa ujumla kwamba   tafsiri hiyo siyo sahihi na ni upotoshaji mkubwa na kwa misingi hiyo  tunapenda kutoa taarifa na ufafanuzi kama ifuatavyo:
1.0. Serikali haijawahi na wala haikusudii kutoza kodi Mafao ya Wanachama na  wala si malengo ya  kifungu cha 56 cha Muswada huu. Ni vema ifahamike kwamba hata katika Sheria za sasa za Mifuko ya Pensheni na Sheria za Kodi, mafao ya wanachama hayatozwi kodi, rejea    kifungu cha 47(3) cha Sheria ya Mfuko PSPF,  kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Mfuko wa GEPF, kifungu cha 90(2) cha Sheria ya Mfuko wa NSSF na kifungu cha 54 cha Sheria ya Mfuko wa PPF. Aidha, masharti na maudhui ya kifungu cha 56 cha Muswada yanafanana kabisa na masharti ya vifungu tajwa hapo juu vikisomwa pamoja na sheria za kodi ambazo ndiyo misingi wa misamaha yote ya kodi nchini.
2.0.   Masharti kuhusu mafao ya Majaji  yamechukuliwa kutoka kwenye Sheria ya Mfuko wa PSPF ambako ni vifungu vya 21 na 22 vya Sheria Hiyo. Hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwenye maudhui ya vifungu hivyo zaidi ya kuboreshwa kwa kutenganisha masharti ya Pensheni na stahili nyingine.    Hivyo taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu mafao ya Majaji ni  upotoshaji  wa  makusudi  unaolenga  kujenga  taswira  potofu mbele ya macho ya Jamii.
3.0.   Eneo la mafao ya Wajane na warithi katika Muswada ni moja ya maeneo ambayo yameboreshwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na    masharti   yalivyo   kwenye   Sheria   za   sasa.   Muswada umebainisha kwa uwazi stahili za Wajane na Warithi pale mwanachama au mstaafu anapofariki.
Tunawashauri na kuwaasa wananchi na Taasisi nyingine kuepuka kutoa maoni ambayo yanalenga kupotosha nia njema ya Serikali katika Muswada huu.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846
Dar es Salaam
22/1/2018

Tuesday, January 9, 2018

Umuhimu wa Kumpunguzia Mtoto Shinikizo la Kufaulu


Ufaulu wa mitihani umepewa nafasi ya pekee katika mfumo wetu wa elimu. Shule zetu, kwa hakika, hazina namna nyingine ya kumwelimisha mtoto zaidi ya kumtaka akusanye, akumbuke na kutumia maarifa aliyonayo kujibu maswali ya mtihani.

Ingawa ustawi wa jumla wa mwanadamu hautegemei eneo hilo moja la ukusanyaji na utumiaji wa maarifa, shule zetu zinaonekana kuamini pasipo mtu kuwa na maarifa mengi hawezi kufanikiwa.

Kasumba hii imetuathiri na sisi wazai. Tunafikiri, kwa mfano, ni lazima mtoto afaulu masomo kwa kiwango cha juu ili afanikiwe. Matarajio haya makubwa yanatufanya tuwaweke watoto kwenye shinikizo kubwa mno la kufaulu tukiamini ufaulu huo ndio kigezo cha ustawi wao katika maisha.

Matokeo yake, tangu mtoto anapoingia shuleni kwa mara ya kwanza mpaka anamaliza, anajikuta katika mazingira ambayo kimsingi hana kazi nyingine zaidi ya kumridhisha mwalimu na mzazi wake kwamba, kama watoto wengine, na yeye anao uwezo wa kukusanya na kukumbuka maarifa.Mazoea haya yanaibua changamoto kadhaa kimalezi kwa watoto.

Kulea tabia ya ushindani

Shule zetu zinathamini wanafunzi wanaofanya vizuri na kudhihaki wale wanaoonekana dhaifu. Mtoto anayefanya vizuri darasani, kwa mfano, ndiye anayependwa na walimu, ndiye anakuwa maarufu, na ndiye anayepata zawadi ya kuwa bora kuliko wengine. Hili ni tatizo na nitaeleza kwa nini.

Kwa muda mrefu tuliamini kumzawadia mtoto mdogo aliyefanya vizuri kuliko wenzake ingekuwa si tu motisha kwake kuongeza jitihada za kufanya vizuri kwa mara mwingine tena, lakini pia ingewafanya watoto wengine kuweka bidii zaidi kwa matarajio ya kupata zawadi kama aliyopewa mwenzao.

Hata hivyo, tafiti nyingi, mfano za Prof. Carol Dweck wa Chuo Kikuu cha Stanford, zinaonyesha utamaduni huu wa kuwapongeza watoto kwa namna inayobagua uwezo wao una kasoro nyingi zinazoweza kukuza mitazamo mibovu kwa watoto.  

Kwa mfano, mtoto aliyezoea kuongoza darasani na kusifiwa anaweza kugeuka kuwa mtumwa wa sifa. Utumwa huu wa sifa unamweka kwenye hatari ya kuwa na tabia ya kuelekeza nguvu kwenye eneo linalomfanya ajione bora na hivyo kukwepa maeneo mengine ambayo, pengine, yanaweza kuwa muhimu katika maisha.

Ikiwa, mathalani, mtoto anajua walimu na wazazi humsifia kwa kufaulu vizuri, mtoto huyu anaweza kukwepa  kushiriki kazi za ndani ambazo anajua haziwezi kumgusa mzazi wake.

Pia, kupongezwa kwa kuwazidi wengine kunaweza kumkatisha tamaa mtoto hasa pale inapotokea ama anafanya vizuri lakini hakuna mtu anayejali au basi kuna mtoto mwingine anayeonekana kumzidi kinyume na vile alivyozoea.

Lakini vile vile, kwa upande wa watoto wanaoshuhudia mwenzao akizawadiwa kwa kuwazidi mara kwa mara, wengi wao hunyong’onyea na kuanza kujiona kama watu duni wasio na uwezo wa kufanya vizuri kama wenzao.

Tafsiri yake ni kwamba, kwa watoto wadogo, hakuna sababu ya msingi ya kuwawekea mazingira ya kuwashindanisha kiuwezo hali inayoweza kuwaingizia dhana ya kushindana hata katika mazingira ambayo hakuna sababu yoyote ya ushindani.

Kudumaza vipaji

Changamoto ya pili ya shinikizo hili kubwa la taaluma kwa watoto, ni kudumaza vipaji ambavyo kimsingi hakuna namna ya kuvipima kwa kutumia mitihani. Kwa kuwa shughuli karibu zote zinazoendelea darasani zinalenga kujenga eneo moja tu la kukusanya na kukumbuka maarifa, mtoto hawezi kuwa na motisha ya kufanya vitu vingine visivyohusiana na masomo.

Matokeo yake mtoto anapokuwa shuleni anakuwa hana kazi nyingine zaidi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Anaporudi nyumbani, hali kadhalika, anakutana na mzazi anayeamini kazi ya msingi ya kufanya kwa mwanae ni kuzingatia masomo.

Mtoto anayeishi kwenye shinikizo la namna hii anapojaribu ‘kuchepuka’ kidogo ili kukuza vipaji visivyotambuliwa na mitihani rasmi ya darasani, anajikuta kwenye mgogoro na mwalimu na mzazi.

Kwa sababu hii, watoto wetu wengi ambao pengine wangeweza kuwa na vipaji vya kila aina, wanaishia kufanya vitu ambavyo mara nyingine haviwafanani.

Kudumaza ukuaji

Shinikizo hili kubwa la kufaulu masomo pia linaathiri mtindo wa kawaida wa maisha ya mtoto. Shule inayotaka mtoto awe bora kitaaluma, kwa mfano, kwa kawaida, itamnyima fursa ya kushiriki shughuli zisizo na kimasomo lakini ambazo kimsingi zingeweza kuwa muhimu kimakuzi.

Mtoto huyu mdogo shauri ya kusoma kwenye shule inayotaka kuongoza kwenye mitihani, hatopata mtu wa kumfundisha kujifanyia usafi wake binafsi, kufagia, kushiriki kazi za mikono kwa sababu tu mitihani ambayo ndio kipimo cha ubora wa shule haina vipengele vinavyopima utu wa mtoto, ushiriki wake kwenye kazi za mikono.

Pamoja na uzuri wa kufaulu masomo, mtoto mdogo wa shule ya msingi, kwa kweli, anahitaji kufaulu pia hata kwenye maeneo mengine yenye nafasi muhimu ya kumsaidia kupata mafanikio katika maisha.

Mbali na kupata alama 95 darasani, kwa mfano, mtoto huyu anahitaji kujifunza umuhimu wa kujali hisia na mahitaji ya wengine, tabia ambayo angeweza kujifunza vizuri zaidi kupitia michezo kuliko vitabu vilivyotajwa kwenye mtalaa.

Kasoro hii ya mfumo wa elimu kutilia mkazo eneo la ufahamu na maarifa kuliko maeneo mengine, imefanya watoto wengi wakose fursa pana ya kujengwa kiroho, kimaadili na hata kupata stadi nyingine muhimu za kimaisha.

Ushauri

Natambua shauku kubwa waliyanayo wazazi kuona watoto wanashika nafasi ya kwanza darasani. Hata hivyo, kama tulivyoona kwa ufupi, shauku hiyo ya kuwa na watoto wenye ‘akili’ isiwafanye watoto wakajikuta wakibanwa mno na hivyo kukosa muda wa kujifunza stadi nyingine za maisha.

Aidha, tunazo sababu za kutosha kuvumilia hata pale tunapoona watoto wetu hawafanyi vizuri darasani. Hakuna ushahidi wa kitafiti unaothibitisha kuwa ufaulu wa sekondari na vyuoni unategemea na ufaulu mkubwa wa ngazi za chini.

Miaka ya awali ina umuhimu mkubwa katika kujenga sura ya maisha atakayoishi mtoto. Tunahitaji kuweka msisitizo mkubwa kwenye kujenga utu, kuwakuza kiroho na kuwafundisha stadi za maisha, kwa sababu hayo ndiyo maeneo yatakayoamua mustakabali wao.


Pia, utamaduni wa kuwashindanisha watoto wa ngazi za chini hauna tija. Tunaweza kuwafanya watoto wakajifunza vizuri bila kuwaambia wameshika nafasi ya ngapi darasani. 

Mbinu za kukuza uwezo wa akili wa mtoto.



Kwa muda mrefu wataalam wengi wa saikolojia ya elimu waliamini uwezo wa akili anaokuwa nao mtu unarithiwa na haubadiliki. Katika kuthibitisha kuwa akili za mtu haziwezi kubadilika, wapo wataalam, tena wengi tu, waliobuni kipimo cha akili za mtu kilichojulikana kama IQ. Kipimo hiki kilitumia mfululizo wa maswali anayoulizwa mtu kujua anawezaje kufikiri, kuelewa na kuchambua mambo.

Lakini kadri utaalam wa kupima utendaji wa ubongo ulivyoendelea kuongezeka, sasa tunaelewa akili za binadamu zinaweza kubadilishwa na mazingira anayokutana nayo mtu.

Mtazamo huu mpya unatupa faida mbili kubwa. Kwanza, unatusaidia kujua mambo yanayoweza kufanyika kubadili uwezo wa akili anazokuwa nazo mtu. Pili, unaongeza wajibu tulionao sisi kama wazazi katika kumwekea mtoto mazingira sahihi yanayoweza kusisimua utendaji wa ubongo wake.

Katika makala haya tutazame mambo manne unayoweza kuyafanya kukuza uwezo wa mtoto kufikiri, kuelewa na kuhambua mambo.

Badili lugha anayojisemea mtoto

Kila mtu anayo lugha ya ndani anayoitumia kufikiri. Lugha hii ya ndani ina kazi kubwa ya kujenga vile unavyojichukulia. Unapofikiri jambo, kwa mfano, unaweza kusema maneno fulani yanayokuhamasisha, kukusifu, kukukosoa, kukutia wasiwasi, mashaka na hata kukukatisha tamaa.

Wataalam wanasema kuna uhusiano mkubwa kati ya mawazo ya mtu na kile anachokifanya. Kama mtoto, kwa mfano, atayaamini mawazo yanayomvunja moyo, matokeo yake yatakuwa ni kushindwa. Mtoto mwenye mawazo yanayomnyong’onyeza hawezi kuzidi mawazo hayo. Kukata tamaa, kujizomea, kujikosea kulikopitiliza, kunamnyima fursa ya kufikiri sawa sawa.

Mzazi jenga mazoea ya kumsemea mwanao maneno yanayomjenga. Tambua mazuri anayoyafanya na yaseme maneno chanya. Usiwe na tabia ya kumkosoa mno mtoto hata kama kweli hajafanya vizuri.

Fikiria mtoto amefanya vibaya darasani. Mzazi wa kwanza anamwambia, “Nikijua tu utafeli. Kwanza huna akili. Naona napoteza tu hela kukusomesha.”

Mzazi wa pili anamwambia, “Kwa namna ninavyokufahamu, uwezo wako ni mkubwa. Najua ukikazana, ukimsikiliza mwalimu na kujisomea, uwezo wa kufanya bidii kufikia uwezo wako halisi.”

Mzazi wa kwanza anaongea kwa hasira shauri ya matajiro makubwa aliyonayo kwa mwanae. Hachagui maneno ya kumwambia mwanae kwa sababu anaamini kufeli mtihani ni kukosa akili. Hajua athari ya maneno yake katika kujenga lugha ya ndani itakayoathiri uwezo wake wa kujituma.

Mzazi wa pili anaweza kuwa na hasira lakini anajua nguvu ya maneno yake. Anamtamkia mtoto maneno yanayomtia hamasa hata katika kufeli kwake. Maneno haya chanya yatajenga lugha chanya itakayokuwa hamasa ya kufanya vizuri zaidi.

Ongeza fursa za mawasiliano

Mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuongeza uwezo wa akili anaokuwa nao mtu. Kuzungumza na mwanao mara kwa mara kunakuza uwezo wake wa lugha, msamiati wake, na hata kusisimua utendaji wa ubongo wake.

Unaweza kushangaa lakini ndivyo wataalam wanavyotuambia. Wazazi waongeaji wenye tabia ya kuzungumza na watoto huwasaidia kuwa na msamiati zaidi.

Lugha ina nafasi kubwa katika kujenga uwezo wa akili.

Bila kujali umri wake, jenga mazoea ya kujadiliana na wanao masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao. Wape nafasi ya kukusimulia yale wanayokutana nayo shuleni, kwenye michezo, mambo wanayoyasikia mitaani, matarajio waliyonayo na hata hofu wanazohitaji kupambana nazo. Fanya mazungumzo yawe utaratibu wa kawaida wa maisha ya hapo nyumbani.

Mfano, mwombe mwanao akuambie siku yake imekwendaje. Mwuulize maswali yanayomtaka ajieleze badala ya kujibu kirahisi ‘ndiyo’, ‘hapana’ na ‘sijui.’ Mruhusu mtoto akuulize maswali na jitahidi kuyajibu kadri unavyoweza.

Mara nyingi mtoto huuliza kutaka kuyaelewa mazingira yake, kuelewa mambo anayoyaona na kukutana nayo katika maisha. Kumbuka muhimu hapa sio majibu unayompa, bali uwezo wa kufikiri, kuelewa, na kuchambua mambo anayoyasikia.

Simulia hadithi

Tangu zamani utamaduni wetu ulitambua umuhimu wa masimulizi kwa watoto. Nyakati za jioni, wazazi walikuwa na utaratibu wa kukaa na watoto wao na kuwasimulia hadithi mbalimbali.

Hadithi hizi, mbali na kukuza ukaribu baina ya wazazi na watoto wao, zilikuza uwezo wa watoto kufikiri. Hadithi, mathalani, zinatumia wahusika wenye tabia na mikakati tofauti kwa kutumia madhari ya kufikirika. Haya yote humfanya mtoto alinganisha anayoyasikia na maisha yake ya kila siku.

Siku hizi desturi hii, hata hivyo, imeanza kupungua. Watoto wanatumia muda mwingi kufanya kazi za kitaaluma ambazo mara nyingine hazihusiani na maisha yao ya kila siku. Mbali na kufifiisha uwezo wao wa kuyaelewa mazingira yao, kazi hizi nyingi zinafunga fikra zao kwenye mambo fulani pekee.

Tunahitaji kufufua desturi ya hadithi kwa watoto. Mbali na kuwasimulia, tuwape nafasi wao wenyewe wabuni hadithi kuwasaidia kujua kuchagua wahusika, kupangilia matukio na kusema wanachokifikiri.

Hamasisha usomaji wa vitabu

Sambamba na masimulizi, mzazi una fursa ya kumhamasisha mtoto kusoma vitabu. Unaweza kuanza kwa kumsomea kitabu chenye hadithi zinazogusa mambo anayokutana nayo kwenye maisha.

Usomaji wa vitabu kwa watoto si tu unaimarisha uhusiano wenu, lakini unaongeza kumbukumbu, uzingativu na hata kukuza msamiati.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa huwezi kukuza tabia fulani kwa mtoto kama wewe mwenyewe huna. Lazima kwanza uanze wewe mwenyewe kupenda kusoma ili mwanao ajifunze.

Swali kwako mzazi, kwa mwaka 2017 ulisoma vitabu vingapi? Je, uliwahi kuonekana ukisoma hapo nyumbani au muda mwingi unautumia kutazama televisheni na kutumia simu?

Je, kuna vitabu vinaonekana kwenye mazingira ya nyumbani?

Lenga kumfundisha mwanao kwa vitendo. Onekana ukisoma ukiwa nyumbani. Kama huna vitabu au magazeti, unavyo vitabu vya dini. Anza na hivyo.

Pia, mnunulie vitabu kama zawadi yake na msomee nyakati za jioni anapojiandaa kulala. Watoto wanapenda sana fursa kama hizi. Kila inapowezekana, mpeleke kwenye maduka ya vitabu na maktaba kupanda mbegu ya mtoto kuwa na urafiki wa kudumu na maandishi.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com

Thursday, January 4, 2018

Zitto Kabwe ahoji Gawio la TZS 300 bilioni kutoka Benki Kuu limetoka wapi?


Thursday, December 28, 2017

RAIS MAGUFULI AWAONYA WATUMISHI WA UMMA KUHUSU TAMKO LA MALI.

Rais John Magufuli amewasilisha fomu ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha fomu leo Alhamisi Desemba 28,2017 ikiwa ni siku moja baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwataka viongozi kuziwasilisha, ameipongeza sekretarieti kwa kazi inazofanya.

Pia, amemtaka Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo Desemba 31,2017.

“Ikifika Desemba 31, ambayo ni siku ya mwisho kwa mujibu wa sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema,” amesisitiza Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa na Ikulu.

Jaji mstaafu Nsekela amemshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimu kujaza fomu hizo.

Amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma si ombi.

“Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila, hapana, sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi,” amesema.

Jaji Nsekela amempongeza Rais Magufuli kwa kuwasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki na tamko hilo, na amekiri kuwa ameonyesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine.

Tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni linatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.IMG_20171228_155354.jpg
Rais Magufuli awasilisha Fomu zake A Rasirimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili wa Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harold Nsekela Makao makuu ya ofisi hizo Mtaa wa Ohio Dar

Tuesday, December 26, 2017

CCM YAMJIBU ASKOFU KAKOBE

Askofu Zakary Kakobe